WANANCHI
wa vijiji vya kuzunguka Hifadhi ya Mbuga ya Taifa ya Serengeti (SENAPA)
wamefichua udanganyifu waliodai kufanyiwa na baadhi ya mawaziri wakati
wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010 kuwa watamiliki bonde la Nyanungu
kwa kumchagua mbunge wa sasa wa Tarime.
Waliwataja mawaziri hao kuwa ni Stephen Wasira (Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais – Mahusiano na Uratibu), Gaudensia Kabaka (Waziri wa Kazi na
Ajira) na mbunge wa sasa wa Tarime, Nyambari Nyangwine.
Wananchi hao walibainisha hayo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira inayoongozwa na Mwenyekiti James Lembeli
ilipowatembelea maeneo hayo na kukutana na wahanga wa Operesheni
Tokomeza Ujangili katika Kijiji cha Kegonga.
Mmoja wa wananchi hao, Kimunye Chacha alisema viongozi hao
waliwadanganya kuwa endapo wangempigia kura Nyangwine wangerudishiwa
Bonde la Nyanungu kuwasaidia katika matumizi ya kilimo na ufugaji.
“Ndugu mwenyekiti tunatambua bonde la Nyanungu ni letu kwani mawaziri
Stephen Wasira, Gaudensia Kabaka na mbunge wetu walituhakikishia kuwa
eneo hilo ni letu na tunashangaa tunaambiwa kuwa ni la TANAPA,” alisema
Chacha.
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Abdulkarim Shah aliyemuwakilisha
mwenyekiti wake, aliwaambia wananchi hao kuwa kamati yake itawasilisha
changamoto walizopatiwa kutoka kwa wananchi hao zilizosababishwa na
Operesheni Tokomeza Ujangili.
Shah aliwatahadharisha kuwa makini na wale wanaohitaji uongozi wakati
wa kampeni, kwani wengi wao wanawadanganya wananchi kwa kujitafutia
kura kwa nafasi wanazozihitaji huku akisema kuwa viongozi hao
waliohusika kuwadanganya hawana budi kuulizwa kwa kile ambacho kinadaiwa
kuchangia kuchochea mgogoro.
Wakati kamati hiyo ikikumbana na changamoto hiyo, Mhifafhi Mkuu wa
Mbuga ya Taifa ya Serengeti (SENAPA), William Mwakilema alisema bonde
hilo ni mali ya TANAPA tangu mwaka 1968 baada ya kupitishwa sheria ya
upanuzi wa mipaka na kuwekwa vipimo vyake iliposainiwa na Rais wa kwanza
wa Tanzania, Baba wa Taifa hayati Juluis Nyerere.
Mwakilema alisema mbuga hiyo ilianza mwaka 1951 na baadae
ilipandishwa hadhi mwaka 1959 ambapo mwaka 1968 ilipanua mipaka yake
kutokana na kujali zaidi mapito ya wanyama hao huku akisisitiza kuwa wao
wanasimamia sheria hiyo na hapaswi mwananchi yeyote yule kuungilia
mipaka hiyo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment