Home » » Chadema yataka deni la Taifa lihakikiwe

Chadema yataka deni la Taifa lihakikiwe

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
 
Siku moja baada ya Serikali kukiri kupanda kwa deni la taifa ambalo sasa limefikia trilioni 27.04, kiasi ambacho kimeanza kuibua mjadala mkali juu ya mwenendo wa uchumi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kunahitajika ukaguzi maalum juu ya suala hilo.
Kadhalika, Chadema kimetaka ufanyike ukaguzi maalum kujua uhalali wa deni hilo na matumizi yake.

Vile vile, Chadema kupitia kwa viongozi wake wakuu maeneo tofauti, kimeitaka Tume ya Taifa  ya Uchaguzi  (Nec) kutoa ratiba kamili ya ukaguzi wa vituo vya wapiga kura na kuanza uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Kauli hizo zimetolewa na viongozi wa chama hicho, Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, walipokuwa wakihutubia mikutano katika maeneo tofauti jana, ikiwa ni mwendelezo wa Mpango wa M4C- Operesheni Pamoja Daima, inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchi nzima.

Akizungumza katika mikutano ya M4C-Operesheni Pamoja Daima iliyofanyika katika maeneo ya Meatu (Mwandoya), Maswa, Malampaka, Bunda (Nyasura) na Musoma mjini jana, Dk. Slaa alisema Watanzania wanahitaji kujua uhalali wa deni hilo na sababu za kufikia kiwango kikubwa hicho na tija ya matumizi yake.

“Tumefikia mahali pabaya…juzi nikiwa Shinyanga huko nilisema kila Mtanzania anadaiwa Shilingi  laki tano (500,000) kutokana na hili deni la taifa ambalo sasa limefikia trilioni 27, lakini naona kuna watu wengine wamefanya hesabu na wamepata ni Shilingi laki sita (600,000), maana yake hata mtoto mdogo huyo hapo asiyejua kinachoendelea naye anadaiwa,” alisema Dk. Slaa.

“Tunajua nchi zote duniani zinakopa, hakuna nchi inayoendelea bila kukopa, suala linakuja unakopa kwa ajili ya nini, hicho unachokopa unakitumiaje. Tunahoji hilo deni limetumikaje? Deni hili litalipwa vizazi na vizazi vijavyo, sasa hao wajukuu wetu watakaolazimika kulipa deni hili watakuwa wanaangalia vitu gani kuwa ni kumbukumbu ya deni ambalo sisi tulikopa,” aliongeza na kuendelea:

“Haiwezekani watu wakope kisha fedha ziliwe, deni lilipwe na wajukuu wetu bila hata kuona zilitumikaje. Tunahitaji ukaguzi maalum ufanyike kwenye deni la taifa, tunataka kujua uhalali wa kudaiwa matrilioni hayo ya fedha.”

Alisema: “Tunataka ukaguzi maalum ufanyike kwa sababu tumeanza kubaini hata matumizi ambayo hizo fedha zinadaiwa kutumika yamekuwa ya ajabu ajabu, mathalani kama ni barabara inajengwa mwaka huu chini ya kiwango, inarudiwa tena kujengwa mwaka ujao chini ya kiwango tena, hivyo itarudiwa tena, kumbe ni mradi wa wajanja kutafuna fedha."

Aliongeza: “Tunataka kuhoji…je; kwa sababu Serikali ya CCM wameanza kuuona mlango wa kuondoka madarakani, wanaanza kukopa, kukopa, kukopa tu ili waiache hii nchi vibaya hivyo utawala ujao urithi madeni makubwa badala ya kuanza kuwatumikia wananchi, uanze kulipa madeni. Tunataka tujue, ndiyo maana tunahitaji ukaguzi maalum,” alisema Dk. Slaa.

Juzi Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema Tanzania inadaiwa kiasi hicho, lakini inakopesheka kwa kuwa deni hilo ni asilimia 28 wakati ukomo wa kukopeshwa ni asilimia 50.

DAFTARI LA WAPIGA KURA
Akionekana kuijibu Nec ambayo juzi ilitangaza kuwa imeshapata fedha kutoka serikalini na hivyo itaanza ukaguzi wa vituo na kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura, kwa ajili ya kura za maoni ya Katiba mpya, Dk. Slaa alisema ni lazima Nec itoe ratiba kuhusu ni lini itakagua vituo vya kupigia kura na lini itaanza kuboresha daftari la kudumu la wapigakura.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa