Home » » Wananchi Rorya wamtaka Rais amtimue DC wao

Wananchi Rorya wamtaka Rais amtimue DC wao

Rais Jakaya Kikwete
 
Viongozi wa CCM wilayani Rorya mkoani Mara, wamemuomba Rais Jakaya Kikwete, kumuondoa Mkuu wa Wilaya hiyo Elias Ole Goloi, kwa madai kuwa ameshindwa kushirikiana na chama hicho kutatua shida za wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa CCM wilayani Rorya Samwel Kiboye, wakati akizindua tawi la chama hicho katika kijiji cha Mchirobi wilayani hapa.
Alidai kuwa mkuu huyo wa wilaya amekuwa chanzo cha kuzorotesha maendeleo ya Rorya akidai tangu ameingia hajawahi kufanya mkutano wa kujadili maendeleo na wananchi, tofauti na kuagiza viongozi wa kata kushughulikia ukusanyaji wa ushuru pekee.

Kiboye aliendelea kumtuhumu mkuu huyo wa wilaya ameshindwa kuwaunganisha Wanarorya, hatua ambayo alisema imefanya wilaya hiyo kugawanyika kwa watumishi wa halmashauri kuwa makundi mawili, likiwamo linalomuunga mkuu na jingine linalomshabia Mkurugenzi wa Maendeleo.

“Sisi CCM Rorya tunasema mkuu huyu wa wilaya hatufai, baada ya kutambua kuwa mie sikubaliani na uovu wake, alikwenda kunishtaki uhamiaji kuwa mimi ni Mkenya na anashangaa nimekipata vipi cheo hiki cha uenyekiti, nilisumbuliwa na uhamiaji kweli,”alisema Kiboye.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo ndiyo wamekuwa wakichukua zabuni za halmashauri huku wakitekeleza miradi hiyo kwa kiwango cha chini na baadhi ya miradi kushindwa kukamilika kabisa na hakuna mtu wa kuwahoji.

Kiongozi huyo wa CCM wilayani Rorya amedai kuwa madiwani hao wamekuwa wakichukua zabuni hizo za utekelezaji wa miradi hiyo na sehemu ya fedha wamekuwa wakigawana na baadhi ya viongozi wakuu wa wilaya kwa maslahi binafsi.

Aliongeza, “nawashangaa hawa viongozi wamekazana na kampeni za uraisi na wakati muda wa kufanya kampeni bado, Rais aliyepo madarakani hajamaliza muda wake lakini wao wanafanya kampeni na kama ukitofautiana nao basi hapo ni chuki ya kufa mtu” alisema Kiboye.

 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa