Kikosi Maalumu cha Polisi kilichotumwa kutoka Dar es Salaam kwa
ajili ya kuongeza nguvu katika msako wa mtu aliyehusika na mauaji ya
watu 10 katika vijiji kadhaa wilayani Tarime, kimewasili na kumeanza
kumsaka mtuhumiwa.
Taarifa ya polisi iliyotiwa saini na Mkuu wa
Operesheni jeshi hilo, Paul Chagonja, ilisema juhudi za kumsaka muuaji
huyo zinaendelea.
“Tumejipanga na tayari timu maalumu ya kuongeza
nguvu katika msako dhidi ya muuaji huyo imeshawasili Tarime,” alisema
Chagonja na kuwataka wakazi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano kwa timu
hiyo.
Mwandishi wa habari hii, alishuhudia ulinzi ukiwa
umeimarishwa katika Mkoa wa Mara. Kazi hiyo inafanywa kwa ushirikiano wa
polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya na Kikosi Maalumu kutoka
Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, jijini Dar es Salaam.
Mauaji hayo ya kikatili, yamezua hofu kubwa
miongoni mwa wakazi wa vijiji vya wilaya hiyo na jana jioni ni watu
wachache tu walionekana wakiwa mitaani .
Polisi wenye mbwa na magari, wamekuwa wakifanya
ulinzi wa doria katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kwa lengo la
kumnasa muuaji.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/ Rorya, Justus Kamugisha, alisema polisi wamejipanga vilivyo kumkabili mtu huyo.
“Msako mkali unaendelea tunashirikiana na polisi
Mkoa wa Mara, huwezi kusema kuna usalama Tarime wakati jambazi bado
hajakamatwa,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele, alisema
ulinzi umeongezwa katika Kata za Turwa, Kitare, Binagi ambako matukio ya
mauaji yametokea.
Aliwataka wananchi kutoa taarifa wanapopata taarifa za mtu wasiyemjua au kumtilia shaka.
Henjewele alisema Serikali inazidi kuongeza nguvu
za ulinzi ili kuhakikisha kuwa mtuhumiwa anakamatwa na kufikishwa mbele
ya sheria.
“Huwa anavaa kofia ya sweta kichwani na moja
anaitumia kukusanyia pesa. Baadhi watu aliowaua kwenye Grosary,
kulitokana na kukataa kwao kutoa pesa alizokuwa anahitaji,” alisema
Henjewele.
Alisema jana, Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa alizitembelea familia za wafiwa na kuzipa pole.
Januari 26, mwaka huu katika Kijiji cha Mogabiri
mtu anayedhaniwa kuwa ni jambazi aliwaua kwa risasi Zakaria Mwita Marwa
(28) na Erick Maranya (24) baada ya kukutana nao njiani.
Usiku wa siku hiyo katika kijiji hicho hicho,
muuaji huyo alimuua, Robert Kisiri (45) baada ya kuvamia Grocery
inayomilikiwa na Chacha Ryoba na kumjeruhi mtu mwingine mmoja.
Januari 27, muuaji huyo alirudi tena katika kijiji
hicho na kumuua kwa risasi, David Mwasi kabla ya kumjeruhi Machungu
Nyamahemba (19) ambaye bado amelazwa katika Hospitali ya Tarime.
Siku hiyohiyo, alimuua pia kwa kumpiga risasi Juma
Nyaitara wakati usiku wa kuamkia Januari 28, aliwaua watu wengine
watatu ambao bado majina yao hayajafahamika. Mtu mmoja alipigwa risasi
wakati akiendesha pikipiki katika Kijiji cha Nkende.
Mauaji hayo yametajwa kuwa ni ya aina yake
kufanywa na mtu mmoja ambaye hata hivyo uwezo waka katika kutumia silaha
haujafahamika.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment