Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Katibu wa Chadema wilayani Bunda, Samuel Alfred, aliyasema hayo jana akieleza kuwa mtoto wa Waziri Wasira amepitishwa na chama chake kupeperusha bendera ya Chadema katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Februari 09, mwaka huu.
Alisema Wasira ambaye ni mwanachama hai wa Chadema ni mtoto wa mdogo wa Waziri huyo.
“Chadema tumempitisha Julius Magambo Wasira kuwa mgombea wa chama chetu katika uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Nyasura, mgombea wetu huyu ni mtoto wa Waziri Steven Wasira na tunaenda kwenye kampeni tukiwa kifua mbele,” alisema.
Alisema kampeni rasmi za uchaguzi huo, zinatarajiwa kuanza Alhamisi hii na zitahitimishwa Februari 08.
Kwa upande wake, kada maarufu wa Chadema wilayani Bunda, ambaye pia alishatangaza kugombea ubunge jimbo la Bunda, Pius Masuruli, aliwaomba wananchi wa Nyasura kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya Chadema, ili kusikiliza sera na mwelekeo wa maisha yao.
Pius alieleza kwamba, kutokana na umuhimu wa uchaguzi huo, atalazimika kusimamisha shughuli zake kwa ajili ya kushiriki kampeni za chama chake anachoamini ndicho kitaibuka kidedea kwenye uchaguzi huo.
Juzi, Wasira alikaririwa akisema kwamba: “Mambo ya kifamilia ni ya kifamilia, baba Wasira yeye ameona awe CCM, lakini mtazamo wangu na wake ni tofauti, mimi naona CCM hainitendei haki.”
Alisema anaamini suluhisho la Watanzania ni Chadema pekee na ukombozi wa kweli utapatikana kupitia Chadema, kwani siyo kandamizi na kwamba akishinda katika uchaguzi huo mdogo, atahakikisha jimbo hilo la Bunda litachukuliwa na Chadema 2015.
Wakati huo huo, Ashton Balaigwa, kutoka Morogoro, anaripoti kuwa juzi chama hicho kiliingia kwa mbwembwe za msafara wa baiskeli, pikipiki na magari wakati wa kumsindikiza mgombea wao, Juma Tembo, kuchukua fomu katika ofisi ya kata ya Tungi na kujigamba kuibuka kidedea katika uchaguzi mdogo wa udiwani.
Huku akiwa ameongozana na pikipiki 14 na magari 10, Tembo alifika kwenye ofisi hizo saa 9 alasiri na kupokelewa na umati wa wana Chadema wa kata hiyo ambao walikuwa wameshika bendera za chama hicho.
"Siku zote Chadema ndio inaibua kero nyingi za wananchi, kikubwa nawaomba wananchi wa kata ya Tungi wanichague niwe Diwani wao niwafanyie kazi katika Baraza la Madiwani la Manispaa,” alisema Tembo.
Naye Kaimu Katibu wa Chadema mkoa wa Morogoro, Boniface Ngonyani, alisema wanauhakika na ushindi kwa maelezo kuwa wananchi wanakikubali chama hicho.
Kwa upande wake, Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Morogoro, Elias Mwalusako, aliwataka wakazi wa kata hiyo kumchagua mgombea wa chama chao ili akalete changamoto kwenye vikao vya halmashauri.
Uchaguzi mdogo kata ya Tungi umetokana na aliyekuwa diwani wa kata hiyo Daudi Mbao kufariki dunia mwaka jana.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment