Home » » ZINDUKA YAINGIA MKATABA WA MILIONI 135

ZINDUKA YAINGIA MKATABA WA MILIONI 135

SHIRIKA la Zinduka limeingia mkataba wa miaka mitatu wa sh. milioni 135 na shirika la The Foundation For Civil Society, kwa ajili ya kutoa elimu ya kijamii kwa viongozi, pamoja na msaada kwa watoto wa mazingira magumu.

Hayo yameelezwa na mkurugenzi wa shirika la Zinduka, lenye makao yake makuu katika kijiji cha Nyamuswa wilayani Bunda, mkoani Mara, Bw. Max Madoro kwenye hafla fupi ya kukabidhi msaada wa vitu mbalimbali, vikiwemo vifaa vya shule na karo kwa watoto waishio katika mazingira magumu na hatarishi.

Bw. Madoro amesema kuwa shirika hilo limeingia mkataba wa miaka mitatu na Taasisi ya The Foundation For Civil Society wa sh. milioni 135, kwa ajili ya kutoa elimu ya kijamii kwa viongozi mbalimbali, pamoja na kutoa msaada kwa watoto waishio katika mazingira magumu katika wilaya za Bunda, Butiama na Tarime.

Amesema kuwa makataba huo unatokana na shirika hilo mwaka 2012 kushika nafasi ya kwanza kitaifa kati ya mashirika 634, katika shindano la kutafuta shirika bora nchini na kwamba kwa ushindi huo lilikabidhiwa kombe na vyeti.

Amesema kuwa hali hiyo inaonyesha wazi kwamba Taasisi kubwa nchini imeanza kutambua utendaji kazi wao kwa jamii ya watanzania.
Aidha, ameongeza kuwa katika kuunga mkono halmashauri ya wilaya ya Bunda, shirika lao linashughulika na shughuli za ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, vyoo, mabweni na kutengeneza madawati na kuyagawa kwenye shule za msingi na sekondari.

Amefafanua kuwa kwa sasa shirika hilo linamalizia ujenzi wa darasa lenye thamani ya shilingi milioni saba katika shule ya msingi Ikizu A na kwamba wananchi wamechangia viashiria na nguvu kazi.

Wakati huo huo, shirika hilo limejenga darasa moja, ofisi ya walimu na vyoo viwili vya wanafunzi  na choo kimoja cha walimu , madawati 20, meza mbili na viti sita, pamoja na kutoa eneo la ekari moja katika shule moja ya awali ya shirika moja liitwalo upendo, ambapo mradi wote umegharimu zaidi ya shilingi milioni 18.1.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa