Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
BAADHI
ya wanawake waishio na Virusi vya Ukimwi, Kata ya Sazira, Wilaya ya
Bunda, mkoani Mara (WAVIU), wamesema bado wanakabiliwa na unyanyapaa
kutoka kwa waume zao.
Wanawake hao waliyasema hayo hivi karibuni
kwenye warsha ya siku mbili iliyofanyika kwenye kata hiyo kwa ufadhili
wa shirika lisilo la kiserikali la The Foundation for Civil Society.
Warsha hiyo ililenga kuwawezesha wanawake hao kuifahamu Sheria ya Ukimwi ya mwaka 2008.
"Tunapokwenda
kupima afya zetu hospitali au kwenye Vituo vya Afya, vipimo vikionesha
kama tumepata maambukizi, licha ya wanaume kukataa kipima afya zao
wanatutelekeza na kutuacha bila matunzo.
"Tabia hii ya kukosa
matunzo mazuri, husababisha maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
hasa kwa wanawake wajawazito au wanaonyonyesha," walisema.
Waliongeza
kuwa, kitendo cha wanaume wengi kutopima afya zao wilayani humo,
kinachangia ongezeko la maambukizi mapya kwa wanawake wengine hivyo
wametoa wito kwa wanaume kuona umuhimu wa kubadili tabia zao kwa kupima
afya.
Akifungua warsha hiyo mgeni rasmi Ofisa wa Maendeleo ya Jamii,
wilayani humo, Bi. Chausiku Mshola, alisema uelewa wa sheria ya Ukimwi
ya mwaka 2008, utawasaidia wanawake hao kuzuia maambukizi mapya.
Alisema
sheria hiyo pia itasaidia kupunguza unyanyapaa kwani itawasaidia
wanawake hao kuelewa nini cha kufanya pale wanaponyanyapaliwa na waume
zao au katika jamii.
Mwezeshaji wa warsha, Bi. Mariamu Mbaraka,
alisema mara nyingi wanawake wanatuhumiwa na waume zao kuwa ndio chanzo
cha maambukizi katika ndoa bila kutambua kuwa, wanawake ndio
wanaofanyiwa ukatili mkubwa kingono.
"Wanaume wamekuwa wakiwabaka
wanawake na kutowapa matunzo jambo ambalo linachangia wanawake kupata
maambukizi kirahisi, hivyo uelewa wa sheria utawasaidia kujua hatua za
kuchukua ili kujikinga na mambo hayo," alisema.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment