Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe
Hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo iliwasilishwa bungeni juzi jioni na Waziri Prof. Maghembe na kuliomba Bunge kuiidhinishia wizara yake Sh. 520,906,475,000 kwa mwaka wa fedha wa 2014/15.
Baadhi ya masuala yanayoashiria kuwa mjadala wa hotuba ya wizara hiyo utakuwa ni wa aina yake ni pamoja na serikali kushindwa kuipatia wizara hiyo kwa wakati Sh. bilioni 138.3 zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji vijijini kwa mwaka wa fedha wa 2013/14.
Hadi kufikia Aprili, mwaka huu, serikali ilikuwa imeipatia Wizara ya Maji Sh. 39,409,607,583 tu kati ya fedha hizo sawa na asilimia 28 ikiwa ni pungufu ya Sh. bilioni 98.9.
Awali, Kamati ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake, Andrew Chenge, iliizuia wizara hiyo kuwasilisha bungeni makadirio ya bajeti yake ya mwaka 2014/15 na kuiagiza serikali kuipatia wizara hiyo kiasi hicho cha fedha mapema iwezekanavyo.
Kamati ya Bunge ilichukua hatua hiyo ikiamini kwamba wabunge wangeiwekea ‘ngumu’ bajeti ya Wizara ya Maji kutokana na kutopewa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji vijijini.
Katika hotuba yake bungeni juzi jioni, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji, Prof. Peter Msolla, alisema serikali ilipaswa kuipatia wizara kiasi hicho cha fedha kilichosalia kabla ya juzi (Mei 31, mwaka huu), ambayo ni siku aliyokuwa akisoma hotuba hiyo.
Hatua hiyo ilimfanya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, kuomba mwongozo wa Spika kama serikali imetekeleza agizo hilo.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alimrushia Pinda, ajibu hoja hiyo.
Pinda alisimama na kueleza kuwa aliiona hotuba ya kamati hiyo na kwamba serikali ilipanga kuipatia wizara hiyo Sh. bilioni 80 kabla ya mwisho wa Mei, mwaka huu.
Hata hivyo, alisema ni matarajio ya serikali kiasi hicho cha fedha kitakuwa kimetolewa hadi ifikapo mwishoni mwa wiki hii.
“Hadi Juni, mwaka huu, tunatarajia tutakuwa tumepata kiasi kingine...itabidi tunyofoe hata kutoka kwenye posho mbalimbali na kama tutashindwa, basi wabunge itabidi mtuelewe tu,” alisema Pinda kwa utulivu.
Kwa kauli hiyo ya Waziri Mkuu Pinda, kuna kila dalili kwamba hakuna uhakika wa kupatikana kwa kiasi chote cha fedha kwa wakati.
Ni kutokana na ukweli huo ndipo inapodhihirika kuwa mjadala wa hotuba ya bajeti ya wizara hiyo utalitikisa Bunge.
Ni dhahiri kwamba wabunge hawataelewa kitu hasa kwa kuzingatia kwamba tatizo la upatikanaji wa maji katika majimbo yao iwe mijini au vijijini, limekuwa likiwatesa wapigakura wao ambao ndiyo mtaji muhimu kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani.
UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI 2014/15
Prof. Maghembe alisema wizara yake imepanga kutekeleza ama kumalizia miradi ya maji 11 katika maeneo mbalimbali nchini.
MRADI WA MAJI TABORA
Prof. Maghembe alisema utafanyika ukarabati wa miundombinu ya maji ya maboresho ya kituo cha maji cha Igombe cha mjini Tabora kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 4.84.
Alisema hadi Machi, mwaka huu, mradi huo ulikuwa umekamilika kwa asilimia 96 na unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa mwezi huu.
MRADI WA MAJI MJINI DODOMA
Prof. Maghembe alisema mradi huo unahusisha ujenzi wa kituo cha kusukuma majisafi kwenda Chuo Kikuu Dodoma (Udom) na ujenzi wa matanki matatu ya ujazo wa lita milioni 12 na ujenzi wa mfumo wa uondoaji wa majitaka utakaogharimu Sh. bilioni 27.7.
Alisema hadi kufikia Machi, mwaka huu, utekelezaji wa mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 54 na unatarajiwa kukamilika Desemba, mwaka huu.
MRADI WA MAJI MJINI SINGIDA
Alisema mradi huo ulihusu uchimbaji wa visima 10, kulaza bomba kuu la maji hadi kwenye matenki na ulazaji wa bomba la usambazaji maji katika eneo la Mandewa ambapo uligharimu Sh. bilioni 32.53.
Miradi mingine ni ya maji Morogoro mjini, Songea Mjini, Mto Ruvuma kupeleka maji Mtwara-Mikindani, mradi wa maji katika miji ya Geita, Sengerema na Nansio, mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria, miradi mipya katika Ziwa Victoria na miradi ya majisafi na usafi wa mazingira katika miji inayozunguka Ziwa Tanganyika.
BWAWA LA KIDUNDA
Prof. Maghembe alisema serikali imekamilisha taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya kuelekea kwenye eneo la bwawa na ujenzi unatarajiwa kuanza baada ya kukamilika kwa tathmini ya ulipaji wa fidia kwa watakaoathiriwa na mradi huo.
MIRADI YA MAJI DAR
Waziri Maghembe alisema wizara yake inajenga na kupanua mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu na ulazaji wa bomba kuu kutoka Mlandizi hadi Kimara kazi iliyoanza Februari 15, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Prof. Maghembe, mradi huo utagharimu Dola za Marekani milioni 99.0 na ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 196 kwa siku kutoka lita milioni 82 za sasa.
Kwa upande wa mtambo wa Ruvu Chini, alisema asilimia 62.87 ya upanuzi imekamilika na inatarajiwa kukamilika mwezi huu.
SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment