Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe, amekemea ubaguzi wa
kikabila kati ya Wajaluo na Wajita, ulioanza kujitokeza katika Kijiji
cha Karukekere, kilichoko wilayani Bunda, mkoani Mara.
Mirumbe, alitoa onyo hilo juzi kwenye mkutano wa hadhara wakati
akihutubia wananchi kijijini hapo, ambapo alisema atakayethubutu kuleta
chokochoko za kikabila atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Alibainisha kuwa dalili za ubaguzi kati ya Wajaluo na Wajita zimeanza
kujitokeza katika kijiji hicho na serikali haiwezi kuzivumilia kwa
sababu zinahatarisha amani.
“Sitaki kusikia tena hali ya ukabila katika kijiji hiki, na wilayani
kwangu kwa ujumla, kama ni suala la uhamiaji haramu linashughulikiwa na
ofisi ya Uhamiaji kuliko baadhi yenu kujifanya ndio wenye jukumu
hilo,” alisema.
Mirumbe, alimuagiza Mwenyekiti wa kijiji hicho, Jogoro Amoni na
Diwani wa Kata ya Namhura, Okore Manase, washirikiane na wananchi
badala ya kuweka mbele itikadi za vyama vya siasa.
“Ninawataka nyinyi viongozi mshirikiane pamoja ili wananchi waweze
kufanya kazi za kujiletea maendeleo na si kila wakati kushikilia
misimamo ya vyama na kulumbana na mnaingiza ukabila eti wahamiaji
haramu… nchi haiwezi kuendeshwa kwa mtindo huo hata kidogo,” alisema.
Katika kikao hicho, diwani na mwenyekiti huyo waliwaomba radhi
wananchi kuwa wao wamechangia kuwepo kwa hali ya kutoelewana kijijini
hapo.
Siku za hivi karibuni ulitokea ugomvi uliosababisha vijana watatu wa
kabila la Wajaluo kujeruhiwa na kulazwa hospitalini baada ya kutokea
ugomvi kwa makabila hayo mawili.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment