Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
“Kwa rasimu hii ilivyo, kama ikipita na kuwa Katiba, nina hakika
viongozi wengi waliotumia vibaya madaraka yao wakati wa uongozi wao na
walioko madarakani, wataishia gerezani na itakuwa mwanzo wa mabadiliko
ya taifa hili.
Tanzania licha ya kuwa na kila aina ya rasilimali,
wananchi wake wameendelea kusota kwa kukosa huduma muhimu za afya,
maji, elimu na miundombinu ya barabara ambayo imeendelea kuwa mibovu.
Lakini rasimu hii itawafuta machozi Watanzania na kuanza ukurasa mpya wa maisha yenye matumaini.”
Hayo ni maneno ya Mwenyekiti wa Vijana Taifa wa
Chadema, John Heche anapofungua mdomo wake kuzungumza na mwandishi wa
makala haya.
Anasema, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, amesikia kilio cha
Watanzania na kuandaa Rasimu ya Katiba itakayowabana viongozi waliokuwa
wakitumia nafasi zao vibaya, huku wakiwaacha wananchi wanahangaika na
ugumu wa maisha.
Heche anaendelea kueleza kuwa Jaji Warioba bila ya
kujali kwamba amekuwa kiongozi ndani ya Serikali ya CCM kwa kipindi
kirefu, akatanguliza uzalendo kulingana na maoni na mapendekezo
waliyoyatoa Watanzania wakati wa kuiandaa rasimu hiyo. “Tume ya Katiba
chini ya Jaji Warioba ilifanya kazi ngumu, kubwa na ambayo haikutegemewa
na Watanzania,” anasema Heche na kuongeza;
“Kwa kipindi kifupi walichopewa wamekuja na rasimu
inayoitetemesha CCM kila wanapoisoma, huku wasijue wanaichakachuaje ili
isipite.”
Heche anabainisha kuwa ukiisoma rasimu hiyo,
utagundua kuwa imeegemea upande wa wananchi, jambo ambalo ni jema,
lakini CCM wanafanya kila njia kuipindisha, jambo ambalo wao
hawatakubali kuona likitokea.
“Kama kuna kitu ambacho Watanzania wanatakiwa
kukipigania kwa nguvu zote, ni rasimu hii, ambayo wao wameipendekeza na
kutokufanya hivyo watakuja kujuta wenyewe,” anasema.
Tunu za Taifa
Heche anasema kwa kuona kuwa taifa limepoteza
mwelekeo, Jaji Warioba ameamua kuweka tunu za taifa ambazo ni Utu,
Uzalendo, Uadilifu, Uwazi, Uwajibikaji, Umoja na Lugha ya taifa ili
viweze kuliongoza taifa.
Anasema Serikali imekuwa ikifanya mambo yake
ambayo yanahusu maslahi ya Watanzania kwa kificho na kuliweka taifa njia
panda kutokana na uzembe na ubinafasi wao. “Jaji Warioba amesema kila
kitu kitafanywa kwa uwazi, kama ni kusaini mikataba basi iwe ni wazi ili
wananchi wajue mikataba hiyo inayosainiwa inawanufaisha akina nani.
Rasilimali ambazo Mungu amelijalia taifa hili kama gesi, madini,
dhahabu, makaa ya mawe na mengine mengi, lakini wananchi bado wanalia
na ugumu wa maisha! Yote haya yamesababishwa na kusaini mikataba kwa
uficho.
Alifafanua kuwa viongozi wengi wamekuwa si
waadilifu, lakini Rasimu hii imezuia matumizi mabaya ya madaraka kwa
kujineemesha na kuacha kuwatumikia wananchi.
“Hivi sasa mtu akipata kazi basi maisha yake
yanabadilika ghafla ndani ya muda mfupi, lakini kwa rasimu hii hakuna
mtu au kiongozi atakayefuja mali ya umma ovyo, kwani atajiweka kitanzini
mwenyewe,” anasema Heche.
Mustakabali wa CCM
Mwenyekiti huyo anasema Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, utahitimishwa na wananchi na wala si chama tawala (CCM).
Anasema hakuna nchi yoyote duniani iliyowahi kuandika Katiba kwa kushirikisha kundi moja.
“Mwisho wa CCM ndiyo umefika, wakiipinga rasimu
hii najua wananchi hawatakubali kuona mapendekezo yao yanatupwa nje
hivyo nao wataitupa katika uchaguzi ujao na hapo ndipo ukurasa mpya
utakuwa umeanza,” anasema Heche na kuongeza:
“CCM imekuwa haina amani tangu Rasimu hiyo
ilipozinduliwa Desemba 30 mwaka jana kutokana na Rasimu nzima kuegemea
upande wa wananchi wakati wakijitazama wenyewe wanaona maji yako
shingoni.”
Heche anasema: “CCM wamekuwa wakisema Jaji Warioba
ni msaliti kwa kuandaa rasimu ambayo wao hawakupendezwa nayo. Sasa mimi
nawaomba wajitokeze kwa wananchi wawaeleze ni kipengele gani kilichomo
ndani ya rasimu hiyo kinachowabana wananchi na kitarudisha nyuma
maendeleo yao pindi wakiipitisha kuwa Katiba.”
Anasisitiza kuwa rasimu hii ni nzuri na inafaa kupitishwa bila vikwazo.
Anafafanua kuwa: “Rasimu inasema ukifikisha miaka
60 hata kama ni mkulima, mchoma mahindi, fundi nguo, baiskeli utatakiwa
kulipwa pensheni ya uzeeni sambamba na wafanyakazi wengine na CCM
wanapinga jambo hili.”
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment