Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Viongozi mbalimbali wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe wakati wa ziara yake Nyamongo
Kumekuwapo malalamiko mengi baina ya wananchi, wenye migodi wa
eneo la Nyamongo wilayani Tarime na askari wa Jeshi la Polisi katika
mkoani Mara.
Mzozo huo umesababisha kutoweka kwa amani , usalama na tuhuma nyingi za mauaji zinazoelekezwa kwa polisi.
Polisi wa kituo cha Nyamongo, hasa wale wanaolinda
mgodi wa dhahabu wa Africa Barrick Gold Mine (ABG) wanalalamikiwa
kuwanyanyasa wananchi kwa kuwapiga na kuwajeruhu kwa risasi na wengine
kuuawa.
Pia, askari walioajiriwa na mgodi ambao
wanajulikana kwa jina la Mobile, nao wanatuhumiwa kuhusika katika mauaji
ya wananchi wanaodaiwa kuingia mgodini kwa nia ya kuokota mawe ya
dhahabu.
Mbali na tuhuma hizo kuelekezwa kwa polisi na
mgodi, Serikali nayo inalalamikiwa kwa kushindwa kutatua kero za
wananchi wake badala yake hutumia nguvu nyingi kupambana na wananchi na
kusababisha uvunjifu wa amani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye pia ni mbunge wa
Nachingwea, Mathias Chikawe akiongozana na waziri kivuli wa Mambo ya
Ndani, Vicent Nyerere ambaye pia ni mbunge wa Musoma Mjini (Chadema) na
mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu walifika Tarime kujua sababu
za kutokuwapo kwa usalama katika eneo la Nyamongo.
“Nimekuja Nyamongo kujifunza kwa sababu nimekuwa
nikisikia kuwa hali ya ulinzi na usalama hakuna; mara watu wanauawa na
polisi; na mgodi nao unadai wananchi wanauvamia. Naombeni nipate taarifa
nijue nini tatizo,” alisema Waziri Chikawe.
Kaimu Meneja wa mgodi ambaye pia ni meneja
machimbo, Jimmy Ijumba anasema kuwa uhalifu na uvamizi wa mgodi ni
changamoto kubwa inayosababisha ugumu katika utawala wa kisheria, na
wananchi wamekuwa wakiiba dhahabu na kuharibu mali na hivyo mgodi
kuingia hasara. alisema wananchi huvamia wakiwa na silaha za jadi.
“Wavamizi huingia mgodi hasa kipindi ambacho shule
zimefungwa kwa kuwa kunakuwa na idadi kubwa ya watu. Zaidi ya watu 100
huvamia. Uvamizi ukizidi shughuli za uzalishaji zinasimama. Mgodi
ukisimama kwa saa moja bila kufanya kazi tunapoteza Dola 24,000 sawa na
karibu Sh30 milioni,” anasema.
Anaeleza kuwa kutokuwapo kwa hali ya usalama
kumesababisha wafanyakazi wa mgodi kutochangia mapato ya biashara za
wananchi kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Wapo baadhi ya wafanyakazi
wameshatekwa, kupigwa na kunyang’anywa mali.
Kwa upande wa miradi, Ijumba anasema mgodi umekuwa
ukisaidia shughuli kama za ukarabati wa shule na kituo cha afya
Nyamongo na maji lakini miundombinu huharibiwa na wananchi na
kusababisha mgodi kuingia hasara kubwa. Alisema jamii inapaswa
kubadilika kwa kuwa kuna kampuni nyingi zilizotangulia lakini
haikutekeleza miradi ya wananchi tofauti na ilivyo sasa kwa ABG.
Aeleza sababu za vifo
Ijumba alikanusha taarifa kuwa watu walio wengi hufia mgodini,
lakini akabainisha kuwa wananchi wenyewe huchomana visu wakati
wakigombania mawe ya dhahabu.
“Huchomana visu na kusukumana kwenye shimo na
wakati mwingine huangukia kwenye shimo lenye urefu wa mita 200-300 na
wasipoelewana hupigana hadi kuuana,” anasema.
Kuhusu Fidia
Meneja huyo anasema kuwa kumekuwa na tatizo la
watu kutegesha nyumba wakizijenga kwa lengo la kufanyiwa tathimini ili
mgodi uwalipe fedha na wanapolipwa huzikataa kwa madai kuwa ni kidogo
ambapo hadi sasa kuna Sh5 bilioni za malipo ya fidia hazijachukuliwa.
Waziri Chikawe na timu nzima yake wakazungukia
maeneo yote ya mgodi kwenye maeneo yanayodaiwa wananchi huruka ukuta na
kuingia ndani kuiba dhahabu.
Pia, akaonyeshwa nyumba zilizojengwa kwa
kutegeshwa kwenye maeneo jirani na mgodi ambako awali hapakuwa na
nyumba. Alieleza kuwa nyumba hizo zilijengwa baada ya kupata taarifa
kuwa kuna maeneo yatafanyiwa thamini kupisha shughuli za mgodi.
Waziri Chikawe alikagua baadhi ya miradi
iliyotekelezwa na mgodi, ikiwa ni pamoja na ukarabati na ujenzi wa Shule
ya Sekondari ya Ingwe, kituo cha afya Nyamongo na ujenzi wa Shule ya
Msingi Nyangoto na Matare.
Mkutano wa waziri viongozi wa vijiji
Waziri Chikawe alikutana na madiwani na viongozi
wa serikali za vijiji saba vinavyozunguka mgodi ili kupata malalamiko
yao ikiwa ni pamoja na kujua tatizo la usalama, kikao kilichofanyika
Shule ya Sekondari ya Ingwe.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja kwa tiketi ya
Chadema, Tanzania Omtima aliilaumu Serikali kwa kumkaribisha mwekezaji
aliyekuta maeneo yakimilikiwa na kuchimbwa na wananchi kisha kuyachukua
bila kuangalia namna gani itawawezesha wananchi baada ya machimbo yao
kuchukuliwa na mwekezaji.
“Chanzo cha kukosekana kwa amani Nyamongo ni
Serikali. Wawekezaji walipewa maeneo makubwa. Asilimia 80 ya Wanyamongo
tangu zamani walikuwa wanategemea dhahabu sasa hawana mahali pengine pa
kupata riziki, hali hiyo imesababisha mwananchi kutojua umuhimu wa
mwekezaji ukizingatia mgodi unachelewa kutekeleza miradi kwa mujibu wa
makubaliano,” anasema Omtima.
Diwani wa viti maalum, Filomena Tontora (Chadema)
anasema: ”Hii Kampuni imeleta migogoro imetuvunjia amani. Enzi za
mwekezaji wa kwanza (kampuni ya Afrika Mashariki Gold Mine, AMGM),
hapakuwa na matukio kama haya. Wazungu walikuwa wanazunguka kila mitaa
wanakula chakula kwenye hoteli zetu.”
Anaongeza kuwa wazungu wale walijiita kwa majina ya Kikurya kama, Bhoke, Chacha, Ghati, Marwa na mengineyo.
Anaeleza kuwa Jeffer alipokuwa akiona mtoto
anachimba dhahabu au siku za shule akikutana na mtoto, anamuuliza ‘mbona
hujaenda shule?’ Mtoto anajieleza. Alisomesha watoto, akiwamo Ghati
Juma ambaye ni mwanasheria wa mgodi, ila tangu Barrick Iwekeze ni
majanga kwani kuna mauaji kila siku mgodini,” anasema Tontora.
Diwani wa Kata ya Kemambo, Wilson Mangure
(Chadema) anawatuhumu polisi wa Nyamongo kwa ukamataji holela, hata kwa
watu wasio na hatia na kuwabambikia kesi za uvamizi mgodini na wizi wa
kutumia silaha.
Diwani wa viti maalumu wa Nyamongo (CCM), Mwajuma
Issa anasema kuwa kazi ya polisi ni kulinda raia na mali zake, lakini
polisi wa Nyamongo wanajiamulia kwenda kukamata watu, wanafukuza watu
nyumbani kwao.
“Wanapekua kwenye magodoro wakikuta simu au pesa
wanabeba wanaondoka navyo na ukikamatwa, hupelekwi kutuoni wanakuomba
pesa Sh100,000 hadi 200,000. Ukikataa ndiyo wanakupeleka kituoni
wanakubambikia kesi za uongo kwa kisingizio kuwa Wakurya ni wakorofi,”
anasema Mwajuma.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyangoto, Elisha
Nyamuhanga (CCM) anasema: “Utawala bora haupo Tarime. Viongozi wa ngazi
za juu wakija Nyamongo viongozi wa serikali za vijiji hatujulishwi hata
ujio wako tumekurupushwa. Mnaonyeshwa na watu wa mgodi miradi iliyo
ndani ya kijiji hata mwenyekiti wa halmashauri hakushirikishwa,”
alisema.
Diwani wa viti maalumu, Loyce Chacha anasema
Serikali ndiyo inawachonganisha wananchi na mgodi kwa kuwa tayari watu
walishafanyiwa tathmini na kikosi kazi kutoka Serikalini. Kwa
kushirikiana na mgodi, walifanya tathmini ili watu wahame maeneo kupisha
shughuli za mgodi, lakini ni mwaka sasa watu hawajalipwa fedha licha ya
kuwa walisimamishwa kuendesha shughuli kwenye maeneo hayo.
Kauli ya majumuisho ya Chikawe
Waziri Chikawe aliwajibu viongozi hao kuwa
malalamiko hayo yamemfanya ajifunze mengi. “Uzuri tumeingia viongozi
wapya, mimi na IGP, ambao tunataka usalama uimarike, polisi wafanye kazi
kwa maadili. Tulishawaambia kuwa polisi atakayeenda kinyume
atawajibishwa msiogope nipigieni simu namba zangu ni 0685777222
nitachunguza nikithibitisha anawajibishwa,” alisema Chikawe.
Alisema baada ya kukamilisha ziara yake ya siku
moja wilayani hapo, amegundua kuna tatizo la uhusiano usioridhisha baina
ya mgodi wa North Mara na wananchi wa vijiji saba vinavyozunguka mgodi
na kusababisha kutokuwepo kwa usalama.
Chikawe anaeleza kuwa kutokuwepo kwa uhusiano
mzuri kumechangia kuwapo kwa migogoro kati ya mwekezaji na wananchi,
hivyo akauomba mgodi kujenga uhusiano ikiwa ni pamoja na kusaidia katika
miradi mbalimbali inayogusa jamii kama afya na maji
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment