Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WATU wawili wakazi wa Kijiji cha Sirorisimba katika Wilaya ya
Butiama mkoani Mara, wamejeruhiwa kwa kuchomwa mishale, baada ya kutokea
ugomvi wa kugombania ardhi kati yao na wakazi wa Kijiji cha Mikomariro
cha wilayani Bunda.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi wilayani Bunda, waliojeruhiwa ni Hamisi
Nyamhanga (38) aliyechomwa na mshale mgongoni na Samson Wambura (36)
aliyechomwa mshale mguuni, wote wakiwa ni wakazi wa kijiji cha
Sirorisimba.
Mwenyekiti wa kijiji cha Sirorisimba, Alexander Makire, aliliambia
gazeti ili jana kuwa tukio hilo limetokea juzi asubuhi baada ya wakazi
wa kijiji cha Mikomariro kuvamia shamba la mkazi wa kijiji cha
Sirorisimba na kuanza kulilima kwa kutumia jembe ya kukuotwa na ng’ombe.
Makire alisema kuwa baada ya mwenye shamba kuwaona watu hao wakilima,
alikwenda kuwauliza kwanini wameamua kufanya hivyo, lakini badala yake
watu hao waliamua kupiga yowe na watu wakakusanyika ndipo vurugu kubwa
zilitokea.
“Majeruhi mmoja amejeruhiwa vibaya na amepelekwa katika hospitali ya
mkoa mjini Musoma,” alisema afisa mmoja wa polisi ambaye hakuwa tayari
kutaja jina lake akidai si msemaji rasmi.
Kufuatia vurugu hizo, jeshi hilo kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya
ya Bunda, walifika eneo la tukio na kuwatia mbaroni watu wawili,
Tulubeth Tundula (32) na Juma Werema (45) ambao wote ni wakazi wa kijiji
cha Mikomariro.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment