Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WALIMU wa shule ya Msingi Nafuba, iliyoko katika kisiwa ndani ya
Ziwa Victoria, Wilaya ya Bunda mkoani Mara, wanafanya kazi katika
mazingira magumu, ikiwa ni pamoja na familia mbili kuishi nyumba moja
yenye vyumba viwili.
Hali hiyo, imebainika juzi baada ya Ofisa Elimu shule za Msingi
Bunda, Jeshi Pembe, kutembelea shule hiyo na kujionea hali halisi ya
mazingira na jinsi walimu wanavyofanya kazi katika mazingira magumu.
Wakitoa kero yao kwa Ofisa Elimu huyo, walimu hao wakiongozwa na
Mwalimu Mkuu, Gatawa Magaji, walisema shule hiyo ina upungufu mkubwa wa
nyumba za walimu, kwani kwa sasa ziko mbili tu.
Walisema kuwa, katika nyumba moja yenye vyumba viwili bila dari,
zinaishi familia mbili za walimu, akiwemo mwalimu mkuu na kwamba, jambo
hilo ni aibu kubwa, hasa ukizingatia juu iko wazi.
Waliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo ya ufinyu wa nyumba hiyo na
aibu kwa familia zao, wamelazimika kupangisha vyumba vingine uraiani
ili watoto wao ambao ni wakubwa, waweze kulala huko.
“Aibu hii unayoiona inatufanya tupange vyumba vingine kwenye miji ya
wananchi, ili watoto wetu wakubwa waweze kulala huko….yaani kwa ujumla
sisi huku tunafanya kazi katika mazingira magumu,” alisema mwalimu
Mbita Maagi.
Walibainisha kutokana na kutokuwepo nyumba za kutosha, ndio maana
walimu wengi wamekuwa hawataki kufundisha kwenye shule hiyo iliyoko
kisiwani.
Walisema kuwa, kwa sasa wapo walimu watano tu wanaofundisha
wanafunzi 570 wa darasa la kwanza hadi la saba, ambako kila mwalimu
hufundisha watoto zaidi ya 100, ambako ikama mwalimu mmoja anatakiwa
kufundisha wanafunzi 45 tu.
Kutokana na changamoto hizo, Ofisa Elimu huyo aliyehamia wilayani
hapa hivi karibuni, pamoja na kusikitishwa na hali hiyo, alisema katika
mipango yake ya kuinua elimu Bunda, atachukuwa hatua zaidi kwa
kuipatia kipaumbele shule hiyo, ili iweze kupata nyumba za walimu
pamoja na kuongeza walimu zaidi.
Pembe, alisema haipendezi kabisa familia za walimu wawili kuishi
kwenye nyumba moja, tena isiyokuwa na dari kwa sababu hiyo ni aibu
kubwa.
Katika hatua nyingine, walimu wa shule hiyo walimpongeza Ofisa Elimu
huyo kwa kuwatembelea na kuona mazingira wanayofanyia kazi, pamoja na
kushuhudia changamoto zinazowakabili, ambako pia wamewataka viongozi
wengine kuiga mfano huo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment