Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KUTOKANA na kero ya wanyama aina ya Tembo kushambulia mazao ya
wananchi, na kuwaingizia hasara, wananchi wanaoishi pembezoni mwa
Hifadhi ya Serengeti wilayani Bunda, wameiomba serikali kutafuta njia
mbadala ya kudhibiti wanyama hao.
Wananchi hao wamependekeza wanayama hao kudungwa sindano za uzazi wa mpango ili wapunguze kuzaliana kutokana na wingi wao.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na mjumbe wa
Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Boniphace
Gitare, wananchi hao walisema kutokana na wingi wa tembo ni vyema
serikali ichukue hatua madhubuti ya kuwazuia.
Walisema kuwa ni vyema wanyama hao hasa majike wakadungwe sindano za
uzazi wa mpango ili wazae kwa majira na wapunguze kushambuli mazao ya
wakulima na kutishia maisha yao.
“Tunaomba serikali itafute njia mbadala kudhibiti wanyama hawa kwa
sababu ni wengi kupita kiasi na wanavamia kwenye makazi yetu, njia
mojawapo tunapendekeza wadungwe sindano za uzazi wa mpango. Mbona
binadamu wanachomwa sindano hizo,” alisema mwananchi mmoja wa kijiji cha
Mariwanda.
Naye Gitare alisema wanyama hao ni rasilimali kwa taifa na kwamba ni
kivutio kwa watalii wanaoingizia nchi mapato, hivyo aliwataka wananchi
hao kuimarisha uhifadhi.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment