Home » » MAJAMBAZI WAUA, WAPORA FEDHA, SIMU

MAJAMBAZI WAUA, WAPORA FEDHA, SIMU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KUNDI la watu zaidi ya 10 wanaosadikiwa kuwa majambazi, wameua watu wawili, kujeruhi wengine kadhaa na kupora fedha za mauzo ya baa na simu katika mji wa Sirari.
Pia, majambazi hao walipiga risasi kioo cha mbele cha gari na kukivunja na pia walipasua tairi kwa risasi. Walivamia pia vibanda vitatu vya maduka na kuviharibu. Walioshuhudia tukio hilo, walisema majambazi hao walikuwa na silaha za moto na za jadi.
Walivamia baa na nyumba ya wageni ya Mzalendo mjini Sirari na kujeruhi watu watatu kwa risasi kisha kupora fedha, simu na kuharibu samani. Pia walivamia vibanda vya maduka, karibu na baa hiyo inayomilikiwa na Ikonde Mrimi na kupora mali na kuviharibu.
Walivamia gari lililokuwa likiingia katika baa hiyo na kupora vitu mbalimbali ikiwemo Sh 500,000. Katika tukio hilo, inadaiwa watu wawili waliojeruhiwa, walifariki.
Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, Lazaro Mambosasa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Alisema upelelezi wa tukio hilo unaendelea. Aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa askari waweze kukamata waliohusika na uhalifu huo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Sirari, Nyangoko Paulo na mashuhuda wa tukio hilo walidai tukio hilo lilitokea saa 2 usiku Ijumaa iliyopita. Akielezea tukio hilo, Paulo alidai kundi hilo likiwa na bunduki na mapanga, walivamia baa hiyo na wawili kati yao waliingia ndani ya baa na kupiga meza kwa fimbo.
Majambazi hao walimwaga vinywaji vyote vya wateja, na kisha wakaanza kupiga risasi na kuamuru kila mmoja atoe alichonacho. Alidai risasi hizo ziliwapata baadhi ya wateja, waliojaribu kupambana nao akiwamo fundi ujenzi, Bhoke Wanchoka aliyepigwa risasi kifuani na kufa papo hapo. Mwingine aliyedaiwa kuuawa hakufahamika.
Wanywaji wengine walijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwilini. Nyangoko alidai wakati majambazi hao wakitoka, walikutana na gari lililokuwa likiingia mahali hapo, papo hapo walimteka dereva wake na kumlazimisha awape Sh 500,000 na fedha za Kenya Sh 20,000 alizokuwa nazo. Baada ya kuiba fedha hizo na za mauzo ya baa, walipiga risasi kioo cha gari hilo na kutokomea.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa