Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WANAWAKE wawili, raia wa Kenya wamehukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini baada ya kupatikana na hatia ya kutoa rushwa kwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Tarime awaachie dhidi ya tuhuma za wizi wa mtoto zilizokuwa zikiwakabili.
Washtakiwa hao, Josephine Nyambare na Wegesa Babere ambao walipelekwa jela mwishoni mwa wiki walishitakiwa kwa kutoa rushwa ya Sh 15,000 za Kenya sawa na Sh 300,000 za Tanzania, kwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Tarime, Hassan Maya amwachie Josephine na kufuta kesi ya wizi wa mtoto iliyokuwa ikimkabili katika Mahakama ya Wilaya Tarime.
Josephine alikuwa akikabiliwa na mashitaka ya kukutwa na mtoto aliyeibwa Tarafa ya Ingwe akimsafirisha kwa gari ndogo ya abiria kwa nia ya kumpeleka Kenya akiwa na nia mbaya na mtoto huyo ikiwamo kwenda kumuuza kwa watu wengine.
Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Tarime, mkoani Mara, Odira Amworo alitoa hukumu mwishoni mwa wiki kwa kuamuru washitakiwa kwenda jela au kulipa faini ya Sh 550,000 kwa kila mmoja kwa kosa la kutoa rushwa ya Sh 300,000 kwa Mkuu wa Upelelezi, Wilaya ya Tarime.
Kwa mujibu wa hatia ya mashitaka, walitoa rushwa kwa mkuu huyo wa Upelelezi awaachie; naye akaamua kuita maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwakamata.
Alisema adhabu hiyo ni fundisho kwa watu wengine ambao wanafanya uhalifu na kutegemea kutoa rushwa ili kuvuruga haki za watu wengine.
Awali, ilidaiwa na upande wa mashitaka kwamba washitakiwa walitoa rushwa hiyo Juni 23 mwaka jana saa 1 asubuhi ofisini kwa mkuu huyo wa Upelelezi.
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment