Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
ZAIDI ya watoto milioni 1.8 wanatarajiwa kupatiwa chanjo, ikiwemo ya surua na rubella, matone ya vitamini A na dawa za minyoo katika Mkoa wa Mara katika kampeni iliyoanza Oktoba 18 mwaka huu.
Hayo yameelezwa juzi na Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Benedict Ole Kuyan, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya surua na rubella, vitamini A na utoaji wa dawa za minyoo iliyofanyika kimkoa kwenye viwanja vya shule ya Msingi Balili wilayani Bunda.
Ole Kuyan, alisema kuwa zaidi ya watoto milioni moja wa kuanzia miezi tisa hadi miaka 15, watapatiwa chanjo ya surua na rubella, watoto zaidi ya 400,000 wa kati ya miezi sita hadi 59 watapewa matone ya vitamin A na watoto zaidi ya 300,000 wa umri wa miezi 12 hadi miezi 59 watapatiwa dawa za minyoo.
Alisema kuwa katika kampeni hiyo Mkoa wa Mara, umeandaa vituo 594 vya kutolea chanjo, ambako katika Wilaya ya Bunda ni vituo 104, Butiama 79, Musoma Vijijini vituo 64, Musoma Manispaa 44, Rorya 88, Serengeti 86, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime 103 na Halmashauri ya Mji wa Tarime vituo 26.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na kuhakikisha kwamba kila mtoto anayestahili kupata chanjo hiyo anaipata kikamilifu.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk. Samson Winani, alisema kuwa chanjo hiyo haina madhara yoyote kwa watoto na kwamba waachane na watu wachache wanaopotosha ukweli kuwa na madhara. Kampeni hiyo itafikia tamati Oktoba 24 mwaka huu.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment