WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewataka wakandarasi wanaojenga miradi ya umeme, kuikamilisha haraka kabla ya Aprili 2015.
Amesema hayo katika ziara yake ya kutembelea miradi ya umeme vijijini mkoani Mara. Profesa Muhongo ambaye ameshazuru wilaya za Musoma, Bunda sasa yuko wilayani Tarime.
Alisema jana kuwa miradi hiyo inatakiwa kukamilika haraka ili wananchi waanze uzalishaji mapema kwa lengo la kujiletea maendeleo na kujikwamua kutoka katika dimbwi la umasikini.
“Serikali imeamua kupeleka umeme vijijini kwa lengo la kufuta umaskini, ikiwa ni pamoja na kuboresha sekta ya elimu kwa shule za sekondari za Kata ambazo ndizo mkombozi wa wananchi wengi waliopo vijijini, sasa hivi tunajenga maabara zinahitaji umeme na vijiji kama hakuna umeme, utategemea watoto kushinda kweli,†alisema Muhongo.
Mhandisi wa Ujenzi, Hussein Ayubu kutoka kampuni ya Derm Helecticet(Ltd), alisema kuwa ifikapo Aprili mwakani, vijiji 27 ambavyo vimetengwa katika wilaya ya Tarime, vikiwemo vya barabara ya Komaswa hadi Nyamongo vitakuwa vimeanza kutumia umeme.
Meneja Utaalamu Elekezi na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Gissima Nyamohanga alisema kati ya mikoa yote 25 Tanzania Bara, vimetengwa vijiji 1,500 kwa ajili ya kupata umeme.
Alisema vijiji hivyo, vimetengewa Sh bilioni 881 ukiwemo mkoa wa Mara, ambao umetengewa Sh bilioni 49 kwa ajili ya vijiji 197 chini ya mpango huo wa awamu ya pili.
Katika wilaya ya Musoma Mjini na Vijijini, ni vijiji 45, Bunda vijiji 45, Rorya vijiji 39, Serengeti vijiji 44 na Tarime vijiji 24. Vyote vitapatiwa umeme kwa awamu hii ya pili, ambapo vimetengewa Sh bilioni 49.
Meneja wa Kanda ya Ziwa, Joyce Ngahyoma, alisema wakati huu wa kupitiwa umeme wananchi watalipa Sh 27,000 kupatiwa umeme, hali itakayowainua katika shughuli zao za uzalishaji na kujikwamua kimaisha kwa kufungua miradi mbalimbali.
Chanzo:Habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment