Hata hivyo, jitihada hizi hivi sasa zinaonekana
kuzorota na dalili zinaonekana katika ubora unaotia shaka wa elimu
inayotolewa kwenye taasisi husika.
Matokeo ya mitihani ya kitaifa katika miaka ya hivi karibuni yanashadadia ukweli wa hali mbaya ya elimu ilivyo shuleni.
Mfano mzuri wa matokeo hayo ni yale ya kidato cha
nne ya mwaka 2012, ambayo yameacha historia ya kusikitisha katika sekta
ya elimu kutokana na idadi kubwa ya watahiniwa kufanya vibaya katika
mitihani yao.
Katika matokeo hayo, asilimia 60 ya watahiniwa
walipata daraja sifuri. Wapo watahiniwa ambao hawakuamini matokeo hayo
kiasi cha wengine kufikia hatua ya kujitoa uhai. Lakini wapo waliokata
rufaa ili warudie mitihani upya.
Kwa kuwa matokeo hayo yalizusha mjadala mkubwa wa
kitaifa, Serikali ililazimika kuunda tume maalumu kuchunguza sababu za
matokeo hayo kuwa mabaya.
Kimsingi, watu wengi wanaamini kuwa miongoni mwa
sababu kubwa zilizochangia matokeo hayo ni migomo ya walimu, mazingira
duni ya kufundishia, kukosekana kwa mtalaa na ukosefu wa walimu wenye
sifa shuleni.
Hata hivyo, Profesa Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam anasema hoja ya mtalaa inayopigiwa kelele kila
kukicha, siyo sababu ya msingi ya kufeli kwa wanafunzi.
Ni wazi kuwa masuala mengine yanayochangia ufaulu
mdogo katika mitihani ni wazazi kutowajibika kusimamia maendeleo ya
taaluma ya watoto wao.
Kwa mtazamo wake, mchango wa wazazi katika ufaulu wa mwanafunzi unachukua asilimia kubwa kuliko muda anaoutumia akiwa shuleni.
Wadau wa elimu wanasema hadi sasa ufuatiliaji wa wazazi ni asilimia mbili tu nchini ukilinganisha na mataifa mengine.
Jukumu la mzazi ni kuhakikisha anafahamu mwenendo
wa tabia za mwanaye shuleni, lakini sasa kazi hiyo wameachiwa walimu na
watendaji wengine.
Sababu kubwa ya wazazi kutokuwa karibu na watoto wao zinaelezwa kuwa ni pamoja na mazingira ya nyumbani.
Jambo la kujiuliza mtoto anaporudi kutoka shuleni
kila siku anakutana na kitu gani? Kama baba ni muuza nyanya basi ni
sahihi akutane na matenga ya nyanya kama ilivyo kwa mwalimu atavyokutana
na vitabu?
Wazazi wengi hawana muda wa kukaa na watoto wao
kujadili masuala ya elimu, badala yake wamekuwa mstari wa mbele
kulalamika mambo yanapoharibika kama ilivyotokea katika matokeo ya
mitihani hiyo.
Haiwezekani mwanafunzi amalize mwaka mzima wa
masomo bila ya mzazi wake kumuulizia kuhusu maendeleo yake. Huku ni
kutowajibika kulikozidi.
Mwanafunzi Edmond Elia wa Shule ya Msingi
Mburahati, anasema anaweza kukaa kipindi kirefu bila ya kuhojiwa au
kukaguliwa maendeleo yake shuleni.
Anasema kila anaporudi nyumbani na wenzake, hutumia muda wake mwingi kwenda katika mazoezi ya mpira wa mguu.
“Sijawahi kuulizwa maendeleo yangu ya shuleni
tangu niingie darasa la saba, ni mara chache hutokea mzee wangu kukagua
madaftari yangu,” anasema.
Baba mzazi wa Edmond ni mfanyabiashara wa maziwa,
hivyo muda mwingi anamtumia mwanawe kumsaidia katika biashara zake
anapotoka shuleni badala ya kumhimiza kujisomea akiwa nyumbani.
Huyu ni mmoja kati ya maelfu ya wanafunzi ambao wazazi wao hawana mpango nao katika maendeleo.
Watanzania tubadilike kwa kuchukua hatua za
kufuatilia kwa ukaribu mienendo ya watoto wetu badala ya kuitupia lawama
Serikali hasa mambo yanapoonekana kwenda mrama katika sekta ya elimu
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment