Home » » ZANZIBAR: WANAWAKE WALILIA MGAWAYO SAWA WA MALI NDOA IKIVUNJIKA

ZANZIBAR: WANAWAKE WALILIA MGAWAYO SAWA WA MALI NDOA IKIVUNJIKA

wanawake wa kijiji cha dunga wilaya ya kati unguja wakiwa na mabango yenye ujembe mbalimbali wakiwa katika maandamano ya kupinga udhalilishaji wa kijinsia.
Wanawake wa Zanzibar wamekuwa na kilio kikubwa cha muda mrefu baada ya ndoa kuvunjika kuhusu mgawanyo sawa wa mali na waume zao ndoa zikivunjika.

Hatua inalenga kuhakikisha kuwa, hawanyanyasiki na kukandamizwa baada ya ndoa zao kuvunyika na kujikuta hawana msaada.

Kuruthum Mohammed, mkaazi wa Mfenesini Unguja ni miongoni mwa wanawake walioolewa , lakini baada ya ndoa yake kuvunjika hana mgao wowote wa mali alioupata kutoka kwa mumewe, waliyechuma naye mali katika ndoa yao.

“ Niliishi na mume wangu katika ndoa kwa muda wa miaka 15. Wakati amenioa, hakuwa hata na nyumba lakini Mungu ametujalia tumechuma wote mali hata kujenga nyumba, lakini sasa ameniacha na watoto wangu bila ya msaada au mgawo wowote kutoka kwake,” alisema kwa masikitiko mama huyo.

Wanawake wengi wanapoolewa alisema kuwa, husaidiana na waume zao kimaisha katika kuchuma mali na kupeana ushauri na maarifa, lakini baada ya ndoa kuvunjika, wanaume huwa hawawajali wanawake na mali hizo hubaki kuwa za mwanaume peke yao.

Alisema, aliyekuwa baba watoto wake waliyezaa naye watoto watano, alimuoa akiwa hana kitu (mali) lakini baada ya kuanza maisha yao ya ndoa, walikuwa wakifanya biashara ndogondogo hatimaye kupata uwezo wa kujenga nyumba, kwa kushirikiana, lakini mwanaume huyo hakuthamini mchango wake.

“ Chanzo cha huyo baba watoto wangu kuniacha, ni baada ya kuoa mke mwengine na kuanza kuondosha mapenzi kwangu bila ya kunijali na watoto wangu niliozaa naye. Baada ya kunipa talaka, alinifukuza katika nyumba na kunitaka nisiondoke na chochote zaidi ya nguo zangu,” alisema Kuruthumu.

Alisema baada ya kuachika katika ndoa yake, alikaa na watoto wake zaidi ya miaka 10 bila ya msaada wowote kutoka kwa baba watoto wake, na mahitaji yote ya watoto alikuwa akiwahudumia yeye.

Baada ya kupata mkasa huo, hakukata tamaa aliendelea kufanya biashara ndogondogo, ikiwemo kuuza dagaa kavu na biashara nyengine akawa anapata fedha za kujikimu kimaisha na watoto wake.

Kuruthum alisema kuwa, maisha yake baada ya ndoa kuvunjika yalitetereka kidogo, ingawa hakuvunjika moyo na kuanza maisha mapya akiwa yeye na watoto wake, lakini sasa ameweza kujenga nyumba yake ambayo hajashirikiana na mwanaume.

“ Nimeamini kuwa, kweli Mungu hamtupi mja wake na hakuna binadamu atakayeweza kuifunga riziki ya mwenzake baada ya kuhangaika zaidi miaka 10 sasa, nimejenga nyumba yangu ambayo naishi mimi na watoto wangu,” alisema Kuruthum.

Aliwanasihi wanawake wenzake wanapokuwa katika maisha ya ndoa kuhakikisha kuwa, kila msaada wanaoutoa wa kimaendeleo kama ujenzi kuandikiana au kuwa na kielelezo cha maandishi endapo mwanamume ataleta ukorofi kuweza kupata haki zao.

Alifahamisha kuwa, kutokana na alivyomuamini aliyekuwa mume wake na kukosa elimu hiyo ya kuweka kumbukumbu kila wanaposhirikiana katika shughuli za kimaendeleo, ndipo yalipomkuta hayo ambayo hakutarajia.

Habiba Ali,mkaazi wa Magogoni mkoa wa Mjini Magharibi Unguja alifukuzwa katika nyumba aliyojenga na mumewe, kwa zaidi ya miaka kumi na tano, mara baada ya kupewa talaka, mumewe alichukua uamuzi wa kumfukuza na kutoa nafasi kwa mke mpya aliyemuoa kuhamia katika nyumba ya shirika.

“ Nilipinga maamuzi ya mume wangu na kumuambia kwamba, siondoki ndani ya nyumba hadi hapo atakaporudisha fedha zangu nilizochangia huku nikimuonesha risiti “ alisema.

Alisimulia kuwa, baada ya baba watoto wake huyo aliyezaa naye watoto watatu, kutaka kumtoa katika nyumba bila ya msaada wowote, mwanamke huyo hakukubali maamuzi hayo, na baba watoto huyo alisalimu amri na kuhama yeye katika nyumba hiyo.

Ukewenza unatajwa kuwa, ni moja ya sababu inayochangia kuwepo kwa wingi wa talaka hata wanawake na watoto kutelekezwa kutokana na sababu mbalimbali.

Miongoni mwa sababu zilizoelezwa kuwa baada ya mwanaume kuoa mke mwingine ni kuporomoka kwa maadili, kutomthamini mke wa mwanzo, wivu na kukosekana kwa elimu ya ndoa kwa wanandoa.

Salma Ali, mkaazi wa Mkokotoni alitelekezwa na mumewe walioishi pamoja kwa zaidi ya miaka 20 na kupata watoto sita, baada ya mumewe kuongeza mke mwingine na kusahau majukumu ya mke wa kwanza.

Alisema walichuma mali pamoja na mumewe, lakini baada ya kupewa talaka aliondoka akiacha kila kitu na kwenda kuishi maisha mapya huku akiachiwa watoto.

“Nilijaribu kudai haki yangu mbele ya Mahakama ya Kadhi, lakini kwa bahati mbaya niliambiwa kwamba, hawashughuliki na masuala ya mgao wa mali kwa wanandoa “ alisikitika Salma.

Miongoni mwa madhila na mateso makubwa yanayowasibu wanawake wengi wa Zanzibar, ni kutelekezwa pamoja na kasi kubwa ya talaka zinazotolewa na wanaume, ambazo zinachangiwa na kuporomoka kwa maadili ya ndoa.

Takwimu katika Mahakama sita za Kadhi Zanzibar zinaonesha kuwa katika mwaka 2012-2013 jumla ya wanawake 1,917 walipewa talaka.

Takriban wanawake wengi  waliopewa talaka, hakuna aliyefaidika na mgao wa mali kutoka kwa waume zao baada ya kuishi kwa muda mrefu na kupata watoto.

Uchunguzi umebaini kuwa, katika miaka ya karibuni wanaume wamekuwa wakitoa talaka kwa wingi kiasi ya kuwepo kwa wimbi kubwa la wanawake waliotelekezwa wakiwa na umri chini ya miaka 21 na watoto wao.

Kuna baadhi ya sheria  zinahitaji marekebisho makubwa ili kwenda na wakati, na kuondokana na matukio ya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto, ikiwemo suala la utelekezaji wanawake na mgawanyo wa mali baada ya ndoa kuvunjika.

Pia imebainika kwamba, taratibu za kufunga ndoa zinatakiwa zifanyiwe marekebisho, ikiwemo wanandoa kupata mafunzo ya ndoa kabla ya kwenda kuishi maisha ya kudumu ya ndoa.

Aidha umri mdogo wa mwanamke au mwanamme kufunga ndoa, nao unachangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa wingi wa talaka, kwa sababu wanandoa wa aina hiyo, hawana elimu ya madhara ya ndoa kuvunjika.

Katibu wa Mufti Zanzibar, Shekh Fadhil Suleiman Soraga alisema ,ndoa nyingi hazidumu hivi sasa, kwa sababu zinakosa maridhiano kutoka kwa wanandoa wenyewe pamoja na wazazi.

Alisema baadhi ya wanandoa wanaamua kufunga ndoa, lakini bila ya kuwashirikisha wazazi, ambao jukumu lao ni kubwa katika familia, huku wengine wakithubutu kuwatafuta marafiki kama mashahidi wa ndoa hizo.

“ Ni kweli lipo tatizo kubwa la kuvunjika kwa ndoa hivi sasa linalosababisha  kuwepo kwa wingi wa talaka, ambalo chanzo chake ni wanandoa kushindwa kuwashirikisha wazee wakati wanapofunga ndoa,”alisema Soraga.

Aidha alisema, mafunzo kwa wanandoa yamekosekana hivi sasa, ambapo Ofisi ya Mufti ipo katika mchakato wa kuwataka makadhi wote wanaofungisha ndoa, kuhakikisha kuwa wanatoa mafunzo, angalau siku mbili kabla ya wanandoa kufunga ndoa.

Soraga alisema “ Hili nalo limekosekana kwa kiwango kikubwa…….watu wanaamua kufunga ndoa, lakini mwanamke au mwanamume hakuna anayejua majukumu yake na haki zake za msingi katika ndoa”.

Sheria ya Mahakama ya Kadhi nambari 3 ya mwaka 1985 inatajwa kuwa na mapungufu mengi, ambayo yanahitaji marekebisho makubwa ili haki za wanawake ziweze kutambuliwa zaidi ,wakati ndoa inapovunjika ambapo kwa sasa mwanamke anaondoka bila ya kupata mgao wa mali baada ya kuishi na mumewe kwa zaidi ya miaka ishirini.

Baadhi ya wanawake wanainyooshea kidole Mahakama ya Kadhi, ambayo wanasema haina meno kuyapatia ufumbuzi matatizo yote yanayohusu masuala ya ndoa na talaka kwa Waislamu.

Kadhi wa Mahakama ya mkoa wa kaskazini B Unguja , Mohamed Kassim alikiri kuwepo, kwa tatizo kubwa la talaka kwa wanandoa ambalo ni moja ya chanzo cha wanawake kuanza kudhalilika na kusambaratika kwa familia  waathirika wakubwa wakiwa watoto.

Alisema mwaka 2013 zaidi ya madai ya talaka na mgawanyo wa mali kwa wanandoa yapatayo 30  yalifikishwa hapo, ambapo wahusika walitakiwa kufikisha suala hilo Mahakama Kuu.

“Tatizo la talaka ni moja ya malalamiko yanayofika katika ofisi yangu ambapo wakati mwengine mwanamke anadai talaka kwa sababu amekosa matunzo kutoka kwa mumewe “ alisema.

Hamisa Mmanga, mwanasheria kutoka Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar  ( ZAFELA ) alisema kwamba, kuna haja ya kuwepo sheria ya ndoa itakayoweka bayana majukumu ya wanandoa na mgao wa mali, wakati ndoa inapovunjika, tofauti na sasa, ambapo wanawake wanapoteza kila kitu na kwenda kuishi maisha mapya wakiwa wageni baada ya ndoa kuvunjika.

“ ZAFELA tuliifanyia utafiti sheria ya Mahakama ya Kadhi na tumegundua kwamba, inakabiliwa na kasoro nyingi zinazoibua malalamiko mengi kwa wahusika ikiwemo wanawake  wanadhalilika kwa kiasi kikubwa na tatizo la talaka,” alisema mwanasheria huyo.

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar ( SUZA ) Dk. Issa Haji Ziddy alisema, baadhi ya nchi za Kiislamu zinazofuata sheria ya Mahakama ya Kadhi, zimeweka utaratibu mzuri, unaotoa nafasi kubwa kwa wanawake kupata mgawanyo wa mali na haki zao zote wakati ndoa inapovunjika, kwa ajili ya kuishi maisha mapya.

Alisema mkataba wa ndoa unahitajika ambao kwa kiasi kikubwa, utasaidia kuweka masharti ya ndoa kwa wanandoa zaidi ,wakati itakapovunjika ambapo maslahi ya mwanamke yatazingatiwa.

“ Kuna nchi za Kiislamu ikiwemo Misri wanayo sheria ya mkataba wa ndoa ambayo imezingatia haki za mwanamke kwa mfano, hata mwanamume anapotaka kuongeza mke wa pili, kwanza unakwenda katika Ofisi ya Mahakama ya Kadhi na kuulizwa unaoa mke wa pili, kwa sababu zipi na haki za mke wa kwanza zitakuwa vipi na uwezo wa kufanya hivyo unao” alisema Ziddy.

Alisema hayo yote ni tofauti na Zanzibar,  ambapo kwa mujibu wa sheria ya Mahakama ya Kadhi mwanamume anaweza kuoa wake wa tatu kwa siku moja na hakuna anayeweza kumuuliza uwezo wake wa kutunza wake hao.

Kadhi mkuu wa Zanzibar, Khamis Haji  alikiri na kusema, talaka zimekuwa zikiongezeka kwa sababu ndoa nyingi zinazofungwa sasa, hazidumu na huku zikikosa maridhiano kutoka kwa pande mbalimbali ikiwemo wazazi.

Wanandoa wanaooana, alisema kuwa kwa bahati mbaya hawajui majukumu yao na haki zinazopatikana katika ndoa wakati inapovunjika ,ambapo hilo linachangiwa na kuwepo ndoa za umri mdogo.

Kwa mfano, alizitaja ‘ndoa za mkeka’ zilizotawala sasa, ambazo nyingi hazidumu kwa sababu zinafungwa bila ya ridhaa, isipokuwa kwa ajili ya kuficha aibu tu, lakini hazina maridhiano pamoja na kupata baraka kutoka kwa wazazi wa pande mbili.

‘Hizo ndiyo sababu kubwa…….ndoa zinakosa maridhiano na maadili yamepungua sana ikiwemo kukosa ustahamilivu tofauti na wazee wetu wanaoishi pamoja na kutenganishwa na kifo tu “ alisema.

Licha ya Tanzania kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa ya kupinga aina za ubaguzi, ikiwemo mkataba wa haki za wanawake CEDEW pamoja na maazimio ya mkutano wa kimataifa wa Beijing China, ikiwemo haki za wanawake za kisheria na kushiriki katika masuala ya kisiasa, lakini bado wanawake wa Zanzibar wanaendelea kunyanyasika.

Akitoa taarifa fupi kuhusu mafanikio yaliyofikiwa na Zanzibar katika malengo ya millennia, ambayo yatafikia tamati mwaka huu, Katibu mkuu Wizara ya Wanawake na Watoto Asha Abdalla alisema, zipo juhudi kadhaa zilizochukuliwa katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake ikiwemo kufanywa marekebisho katika mswada wa Mahakama ya Kadhi, kwa ajili ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake
“Wizara inaendelea na mikakati ya kuhakikisha sheria zote zinazowakandamiza wanawake zinafanyiwa marekebisho makubwa ikiwemo hii ya Mahakama ya Kadhi ,ambayo ipo katika hatua za mwisho” alisema Abdalla.
 
CHANZO: NIPASHE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa