Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mbunge wa Viti Maalum CCM mkoa wa Mara, Ester Bulaya.
Hali
imeendelea kuwa tete ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya
aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum CCM mkoa wa Mara, Ester Bulaya,
kutangaza kukitosa kwa kutangaza uamuzi wake wa kutogombea ubunge kwa
tiketi ya chama hicho.
Bulaya ambaye alikuwa mbunge machachari kabla ya Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kuvunjwa na Rais Jakaya Kikwete, hivi karibuni ,
ametangaza kutogombea ubunge kupitia CCM wakati akizungumza na NIPASHE
baada ya kazi ya kuchukua fomu ndani ya chama hicho na kurejesha
kuhitimishwa rasmi nchini jana.
Tangu mwanzo mwa mwaka huu, Bulaya alitangaza kugombea ubunge
katika Jimbo la Bunda kupambana na Mbunge aliyemaliza muda wake ambaye
ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.
Bulaya amekuwa kada wa pili ambaye alikuwa mbunge kutangaza
kutogombea ubunge kwa tiketi ya CCM, mbunge wa kwanza kutangaza
kutogombea ubunge kupitia CCM baada ya James Lembeli, ambaye alikuwa
Mbunge wa Kahama.
Hata hivyo, Bulaya hakuweka wazi kama ana mpango wa kuhamia chama
kingine cha siasa na kutimiza azma yake ya kuwania ubunge katika
uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Ingawa Bulaya hajaweka wazi, vyama ambavyo vimekuwa vikitajwa
kusubiri makada kutoka CCM kujiunga navyo ili wawanie ubunge ni Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo na Chama cha
Wananchi (Cuf).
M/KITI MONDULI APIGILIA MSUMARI
Wakati ikiwa hivyo kwa Bulaya, hali bado si shwari ndani ya CCM
Wilaya ya Monduli baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Monduli, Edward Sapunyo, Kupigilia msumari wa mwisho na kubariki hatua
ya madiwani wake 20 kukihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza mjini hapa jana, Sapunyo ambaye alikuwa Diwani wa kata
ya Moita, alisema madiwani wake hawawezi kusubiri hadi Mbunge wa Jimbo
la Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, atoe kauli kuhusu
hatma yake ya kisiasa ndani ya CCM.
Kauli ya Sapunyo ambaye hatagombea udiwani uchaguzi wa mwaka huu,
imekuja siku moja baada ya madiwani 20 wa jimbo hilo kutangaza rasmi
kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema).
“Hatuwezi kuona baba yetu anapigwa na kuanguka chini halafu
tusubiri kauli yake, ni lazima tuchukue hatua mara moja…hii haivumiliki,
kitendo alichofanyiwa (Lowassa) na vikao vya CCM mjini Dodoma hivi
karibuni kwa kukata jina lake pasipo kumpa haki ya kumsikiliza siyo cha
kidemokrasia,” alisema.
Lowassa na makada wenzake wa CCM 38 walichukua fomu ya kuomba
ridhaa ya kuteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera ya kuwania kiti
cha urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka
huu.
Katika kinyanyang’anyiro hicho, jina la Lowassa na wenzake
yalikatwa katika hatua ya mwanzo, hali ambayo imezua malalamiko kwamba
ikidaiwa kuwa hawakupewa
nafasi ya kuhojiwa.
“Tumepigwa, tumesambaratika (CCM) Monduli, hatuwezi kuchukua fomu
za kuomba kugombea au kutetea nafasi zetu ndani ya chama hiki, tumehamia
Chadema,” alisema.
Akizungumzia hali ilivyo, Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli, Elisante
Kimaro, alidai kuwa siyo kweli kwamba madiwani wote wamekihama chama
chao.
Kimaro alidai kuwa baadhi ya madiwani waliotangaza kukihama chama hicho wameanza kusalitiana.
Alisema madiwani hao ambao anawaita ni makada baada ya Baraza la
Madiwani la Halmashauri ya Monduli kuvunjwa, walifanya mkutano kwa
kushawishiwa na mmoja wao.
Alisema ushawishi huo unatokana na uchu wa madaraka alionao kwa
kuwa tayari wananchi wa Jimbo la Monduli, wanapenda aliyekuwa Mbunge wa
Viti Maalum CCM, Namelok Sokoine, kuchukua fomu za ubunge wa jimbo hilo.
Alisema kutokana na ugumu huo, diwani huyo wa zamani ametumia mbinu
ya kuwarubuni wenzake wakihame chama hicho ili agombea ubunge kwa
tiketi ya Chadema.
“Huo ni uchu wa madaraka aliyo nayo,” alisema na kuongeza: “Diwani huyo hakubaliki na wananchi wa kata yake."
Alidai kabla ya kutangaza kukihakama chama hicho, madiwani hao
walikuwa wameshafanya kikao na kuweka azimio la pamoja la kuondoka CCM,
lakini juzi walipotangaza uamuzi wao, walijikuta wapo madiwani watatu.
Alisema baadhi ya madiwani walimfuata ofisini kwa lengo la kumuomba
radhi lakini yeye aliwaambia waende kuwaomba radhi wananchi katika kata
zao.
“Madiwani wachache walikuja hapa ofisini kuomba radhi kwa Katibu wa
CCM Wilaya, nikawaambia waende kuwaomba radhi wananchi,” alisema.
Akimzungumzia Lowassa, alisema anachoelewa ni kwamba hajatoa tamko
lolote kama anakihama chama hicho kama inavyodaiwa na baadhi ya watu na
mitandao ya kijamii.
“Bado tuna imani na Lowassa kuwa ni CCM, mpaka sasa hajatoa tamko
lolote kukihama chama, lakini ikiwa vinginevyo itakuwa hatari kubwa,”
alisema.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment