Home » » WANAWAKE JITOKEZENI KWA WINGI KUPIGA KURA - MAMA SALMA KIKWETE‏

WANAWAKE JITOKEZENI KWA WINGI KUPIGA KURA - MAMA SALMA KIKWETE‏

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Na Anna Nkinda – Tarime
 Wanawake wilayani Tarime wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu itakapofika na wachague viongozi watakaowaona wanafaa ambao watawaletea  maendeleo.

Rai hiyo imetolewa leo na  Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanawake wa wilaya hiyo iliyopo mkoani Mara katika ukumbi wa mikutano uliopo katika hoteli ya CMG.

Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini alisema kupiga kura ni haki ya kila mtu hivyo basi haitakuwa busara kwa  wanawake hao kuharibu kura zao kwa kukaa majumbani siku ya uchaguzi ikifika bali waende kupiga kura katika vituo walivyojiandikisha .

“Kura ni siri ya mtu, wewe ndiye unayefahamu kiongozi gani wa kumchagua nawasihi chagueni viongozi wazuri na siyo bora viongozi, wahimizeni wanawake wote waliojiandikisha washiriki kupiga kura kwani kura zenu yako ndiyo itakayokupatia kiongozi unayemtaka”, alisema Mama Kikwete.

Alisema siasa siyo uadui wala ugomvi bali ni mchakato wa kidemokrasia na kuwataka wagombea wote kunadi sera zao kwa kufuata utaratibu na amani kwa kuzingatia kanuni na sheria zilizopangwa na tume ya Taifa ya Uchaguzi ili utulivu na Amani viendelee kutawala nchini.

Aliwasihi, “Msigombane kutokana na tofauti ya itikadi za vyama vya siasa, angalieni siasa zisiwafarakanishe ikafika hatua mkashindwa hata kusaidiana ikiwa ni pamoja na kushindwa kuzikana kumbukeni nyinyi ni ndugu wa wilaya moja ya Tarime”.

Aidha Mama Kikwete aliwataka  wanawake hao kujenga tabia ya  kujiwekea akiba Benki kutokana na fedha wanazozipata katika kazi wanazozifanya kwa kufanya hivyo wataweza kukopa fedha nyingi ambazo watafanyia shughuli za maendeleo na hivyo kujikomboa kiuchumi.

“Unganeni  pamoja ili muweze kujikwamua kiuchumi, simameni katika majukwaa teteeni haki zenu, pingeni mila zilizopitwa na wakati ambazo zinamkandamiza mwanamke na hivyo kumrudisha nyuma kimaendeleo kwa kufanya hivyo mtaweza kujikomboa  kutoka katika hali ya unyanyasaji”,alisisitiza .

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa