Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Anna Nkinda – Tarime
Mgodi wa
dhahabu wa North Mara uliopo wilayani Tarime umetumia kiasi cha shilingi
bilioni 1.7 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Sekondari JK Nyerere pamoja na
nyumba za walimu.
Ujenzi wa shule hiyo
iliyopo kijiji cha Nyamwaga
kinachopakana na mgodi huo umeenda sambamba na ununuzi wa samani za ofisi
za walimu, madarasa na maabara.
Hayo yamebainishwa leo na
Meneja wa Mgodi huo unaomilikiwa na kampuni ya ACACIA, Jimmy Ijumba wakati wa uzinduzi wa Shule hiyo
uliofanywa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete na kuhudhuriwa na viongozi wa
Serikali, vyama mbalimbali vya siasa, wanafunzi na wananchi.
Ijumba alisema shule hiyo
imejengwa kwa awamu ambapo kwasasa
zimekamilika awamu mbili ambazo wigo wake ni madarasa nane, nyumba za walimu
sita zenye vyumba vya kulala vitatu, stoo, jiko, bafu, tanki la maji pamoja na
uzio, jengo la utawala, maktaba, maabara mbili, vyoo vya walimu na wanafunzi vyenye
matundu 33.
Aidha Mgodi huo umenunua
kompyuta za wanafunzi na walimu, photocopier machine, printer, projector na scanner
kwa ajili ya shule hiyo.
Alifafanua kwamba ujenzi
wa shule hiyo umekuwa ukitekelezwa kwa awamu kutokana na shule kuwa mpya kwani ina
kidato cha kwanza na cha pili na kama majengo yote yangejengwa kwa wakati mmoja
yangekosa matumizi.
“Awamu ya tatu ya ujenzi
wa shule hii utatekelezwa mwakani kwa kuhusisha madarasa manne, bwalo la
chakula na chumba cha kupumzikia wagonjwa”, alisema Ijumba.
Kwa upande wake Mama
Kikwete aliipongeza kampuni ya ACACIA
kwa kuchangia jitihada za Serikali za kuboresha elimu kwa watoto na
kusema kuwa mfano huo unapaswa kuigwa na makampuni mengine hapa nchini.
Alisema njia pekee ya
kupambana na ujinga, maradhi na umasikini ni kuwapeleka watoto shule kwani wao
ndiyo tegemeo la wazazi, nguvu kazi na rasilimali ya taifa. Wakielimishwa
watakuwa wanawatengenezea njia ya kujikomboa katika Nyanja za kijamii na
kiuchumi na watakuwa msaada mkubwa kwa wazazi wao pindi watakapokuwa wazee.
Mama Kikwete alisisitiza,
“Watoto wote wa kike na wa kiume wanahaki sawa ya kupata elimu kuanzia ya awali
hadi ya juu, hakikisheni wanakwenda shule kusoma hasa masomo ya sayansi ambayo
ni rahisi ukilinganisha na masomo mengine.
Tuachane na mila
kandamizi za kufikiria kwamba watoto wa kike ni wa kuolewa tu na wa kiume ndiyo
wa kusoma kama wazazi ni lazima tutambue kuwa kufanya hivyo ni kuvunja haki ya
mtoto yatupasa kutambua kuwa ukimuelimisha mtoto wa kike unaelimisha jamii nzima,”.
Alitoa wito kwa kampuni
ya ACACIA kuendelea kukamilisha mikataba waliyokubaliana na vijiji
vinavyowazunguka na kuendelea kuisaidia jamii siyo ile tu inayoizunguka migodi
bali hata iliyopo nje kulingana na mahitaji yao kwani Serikali inaamini
rasilimali za Taifa zinapaswa kunufaisha wananchi wote bila kujali wapi zilipo.
“Rai yangu kwenu ni
kuendelea kuimarisha mahusiano na wananchi ,mgodi uendelee kuwasaidia
wachimbaji wadogowadogo kiteknolojia, ujenzi na vifaa, tafuteni namna nzuri zaidi
ya kuwawezesha vijana na kina mama wanaotafuta dhahabu katika maeneo
mnayohifadhi ambayo mmewaruhusu kufanya hivyo
ili shughuli hiyo iwe rasmi na endelevu”, alihimiza.
Akisoma risala ya
wananchi wa kijiji cha Nyamwaga
Mwenyekiti wa kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 10,000 Getende Sagirai
alisema kijijini hapo kuna shule moja ya
sekongari ya JK Nyerere iliyojengwa na mgodi wa North Mara.
Sagirai alisema katika sekta
ya elimu wanakabiliwa na upungufu wa
walimu wa masomo ya sayansi, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, maabara,umeme
mashuleni,maji, vyombo vya usafiri, mabweni, mabwalo, kumbi za mikutano,
viwanja vya michezo na ukosefu wa uzio katika maeneo ya shule pamoja na nyumba
za walimu.
“Tunaushukuru uongozi wa
kampuni ya ACACIA kwa mahusiano mema ambayo yanadhihirikashwa na vitu halisi visivyoweza
kuhamishika wala kusahaulika na vizazi kwa vizazi vyote vya Nyamwaga.
Vitu hivi ni usambazaji
wa maji safi kwa matumizi ya binadamu, ujenzi wa barabara, ukarabati wa shule
ya msingi Nyamwaga unaoendelea, mradi wa Can educate unaofadhili watoto wanaotoka
katika mazingira magumu ili wapate elimu, ujenzi shule ya sekondari, na ajira
zinatolewa kwa vijana wa eneo hili katika
mgodi”, alisema Mwenyekiti huyo wa Serikali ya kijiji.
Mradi wa ujenzi wa shule
ya JK Nyerere ni moja kati ya miradi ya kijamii katika kijiji cha Nyamwaga
inayotekelezwa kwa ufadhili wa mgodi
kama ilivyoainishwa kwenye mkataba wa manufaa ya vijiji (VBIA) uliosainiwa kati
ya mgodi na kijiji mwezi Februari 2012.
Miradi mingine ni ya
sekta ya maji, afya, elimu, barabara za jamii, umeme na uchumi.
0 comments:
Post a Comment