Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mke wa Rais
na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi,CCM, Mama Salma Kikwete
akiwapungia mkono viongozi na wanachama wa UWT wa Mkoa wa Mara wakati akiwasili
kwenye ukumbi wa Musoma Community Centre kwa ajili ya mkutano wa ndani na
wanachama hao tarehe 3.10.2015.
Umati wa
wajumbe wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa Mkoa wa Mara wakimsikiliza kwa makini Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete (hayupo pichani) wakati alipokuwa akiongea nao Mjini
Musoma tarehe 3.10.2015.
Mke wa Rais
Mama Salma Kikwete akizungumza na wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)
wa Mkoa wa Mara wakati alipokutana nao kwenye ukumbi wa Musoma Community Centre
tarehe 3.10.2015.
PICHA NA JOHN LUKUWI.
Na Anna Nkinda- Maelezo, aliyekuwa
Musoma
Wanawake wa
mkoa wa Mara wameaswa kushirikiana kwa pamoja katika shughuli za maendeleo bila
kuangalia tofauti ya itikadi zao za vyama kwa kufanya hivyo watajiletea maendeleo yao kama wanawake.
Rai hiyo imetolewa jana
na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanawake wa mkoa huo
katika ukumbi wa mikutano wa Musoma Community Center (MCC) uliopo mjini Musoma.
Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini alisema
masuala yanayowahusu wanawake hayana
itikadi za vyama kwani maendeleo ni ya wote, katika mambo ya msingi waungane na
kuwa kitu kimoja wasitenganishwe na watu.
Alisema ili wanawake
waweze kujiletea maendeleo ni lazima
washikamane, wafanye kazi kwa umoja na
kutumia fursa zilizopo kwani Serikali
inasehemu yake ya kuwaleta maendeleo lakini maendeleo mengine yanahitaji jitihada
zao binafsi.
“Sisi kama wanawake
tunafanana kwa kila kitu tofauti iliyopo ni wajibu wa kila mmoja wetu katika
jamii yake, shirikini kuchangia shughuli za maendeleo kama ujenzi wa barabara
na shule kwa ajili ya watoto wetu na kuchangia huduma ya afya ili tuweze kupata
huduma bora”.
Msiache kuzitumia fursa
zilizopo wasimamieni watoto wa kike
wasome kwani wakiwa na elimu wataweza kujiajiri au kuajiriwa, wengine watakuwa viongozi
wazuri miaka michache ijayo watawasaidia siku za baadaye”, alisisitiza Mama
Kikwete.
Aidha Mama Kikwete alitumia
nafasi hiyo kuwaaga wanawake hao na kuwashukuru kwa jinsi walivyokuwa wanamtia
moyo katika kipindi chote cha miaka 10 ya utawala wa mme wake Rais Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete jambo ambalo lilimpa ujasiri katika kufanya kazi zake za
kuwasaidia wanawake na watoto wa Tanzania.
Mama Kikwete alisema, “Kazi
yangu ninayoifanya kama mke wa Rais nimeitekeleza nilisema nitawasomesha watoto
wa kike wanaoishi katika mazingira magumu nimewasomesha, nimejenga shule ya
watoto wa kike, nimewainua wanawake kiuchumi na nimesaidia kuimarisha afya ya
mama na mtoto”, alisema Mama Kikwete.
Katika mkutano huo
wanawake walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali na kuzitaja kero na
changamoto zinazowakabili katika maisha
yao kama vile upatikanaji wa maji, uongozi, uchumi na elimu.
Kwa upande wake Theresia
Chacha ambaye ni mkazi wa Nyamagugu wilaya ya Rorya alimshukuru Mama Kikwete kwa
kumsomesha mtoto wake wa kike aitwaye Paschazia ambaye yupo kidato cha nne katika Shule ya
Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo Rufiji Mkoani Pwani.
“Mama Kikwete anasomesha
watoto 15 kutoka mkoa wa Mara katika shule yake, mwanangu ni mmoja wa watoto hao, anamgharamia
kila kitu hata nauli mama huyu analipa mimi silipo chochote”.
Miaka yote hiyo sijawahi
kumuona ndiyo namuona leo nakushukuru sana Mama, Mwenyezi Mungu akubariki
naomba kiongozi ajaye aige mfano wako wa kuwasidia wanawake na watoto wa
Tanzania”, Mama Chacha alishukuru.
Naye Anastazia Sangarya
mkazi wa kata ya Mwisege ambae ni mjasiriamali alizitaja changamoto
wanazokutana nazo kuwa ni pamoja na kupanda kwa ada ya ushiriki wa Maonyesho ya
kimataifa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere maarufu kama sabasaba yanayofanyika
kila mwaka jijini Dar es Salaam kutoka shilingi 50,000 hadi 100,000.
Mama Anastazia alisema, “Sisi
wanawake wajasiriamali tunaumizwa na ada kubwa ya ushiriki wa maonyesho ya
sabasaba kwani tukishiriki licha ya kulipa kiingilio bado kuna gharama ya nauli
na malazi”.
Kwa upande wa mikopo tunayokopa benki riba yake ni kubwa na kama
ikatokea umechelewa kurejesha kutokana na matatizo ya kifamilia benki
haikuelewi tunakuomba mama yetu utusaidie kutatua changamoto hizi ambazo
zinarudisha nyuma maendeleo ya wanawake wajasiriamali wa mkoa huu,”.
Mama Kikwete aliahidi
kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili wanawake hao na kuwataka viongozi wao
kuitisha mikutano ya mara kwa mara itakayosaidia kutatua kero zinazowakabili.
0 comments:
Post a Comment