Home » » ELIMU BURE YAVUTA WANAFUNZI WENGI.

ELIMU BURE YAVUTA WANAFUNZI WENGI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SHULE ya sekondari ya kata ya Sirari mkoani Mara, inakabiliwa na upungufu wa madarasa kutokana na kuzidiwa na wanafunzi baada ya elimu kutolewa bure na serikali.
Kutokana na hatua hiyo, mwitikio wa wazazi na walezi wa wanafunzi kutii agizo hilo la serikali la elimu bure, shule za msingi na sekondari zimewahamasisha kuwapeleka kwa wingi watoto wao darasa la awali na wale waliofaulu darasa la saba mwaka jana.
Uongozi wa shule hiyo umelazimika kuitisha kikao cha dharura cha wazazi kutafuta mbinu za kusaidia juhudi za serikali katika suala hilo. Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo anayemaliza muda wake, Joel Mwita, alisema kwa sasa darasa moja linatumiwa na wanafunzi 80 badala ya wastani wa wanafunzi 45.
Alisema wanafunzi 400 wameripoti shuleni hapo.
Alisema miongoni mwa mikakati iliyotumika na uongozi pamoja na bodi ya shule na kusababisha mwitikio chanya wa wazazi kupeleka watoto shule, ni pamoja na kuhamasisha jamii kupitia wazee wa mila kukomesha ukeketaji kwa watoto wa kike na badala yake kuwapeleka shule.
“Kwa sasa idadi ya wanafunzi wasichana imeongezeka kulinganisha na mwaka 2015, tumefanikiwa kusajili zaidi ya wasichana 200 kuanza kidato cha kwanza kwa kuwa kila baada ya miaka miwili jamii hushiriki zaidi katika tohara na baadaye kuwaozesha wasichana wao kwa lengo la kupata mahari,” alisema.
Aliomba wazazi waharakishe upatikanaji wa bodi ya shule baada ya ile iliyokuwa chini yake kumaliza muda wake.
Lengo ni kusimamia rasilimali za umma zikiwemo fedha katika taasisi hiyo ili kuhakikisha fedha itakayotolewa na serikali mwaka huu inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Alisema hatua hiyo itawezesha usimamizi mzuri wa fedha za umma na kuepusha tabia ya baadhi ya wakuu wa shule ambao ni makatibu wa bodi hizo, kutumia vibaya fedha za umma zinazopelekwa kama ruzuku ya kufidia michango iliyofutwa kuanzia mwaka huu.
CHANZO ; HABARI LEO.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa