Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wanafunzi
wa Shule ya Msingi Nyabitocho, Tarime mkoani Mara, wanalazimika
kujisaidia katika mashamba ya shule kutokana na shule hiyo kuwa na
matundu machache ya vyoo.
Baadhi ya wanafunzi hao pia wanalazimika kujisaidia katika choo cha
shule kwa kupeana zamu baina ya wale wa jinsia ya kike nay a kiume,
hali ambayo inawaweka katika mazingira magumu.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Sylvester Daniel, alisema jana kuwa
tatizo la choo shuleni hapo lilianza tangu Aprili, mwaka jana, baada ya
kilichokuwapo kubomoka.
Alisema shule hiyo yenye wanafunzi 750, ina choo chenye matundu
manne tu, hali ambayo imekuwa ikiwalazimu kupata huduma hiyo muhimu kwa
shida, huku wengine wakilzimika kujisitiri katika mashamba ya shule
yaliyoko eneo hilo.
Kwa mujibu wa Daniel, kitendo cha wanafunzi kujisaidia ovyo hadi
kwenye mashamba ya shule, kimesababisha baadhi yao kuumwa matumbo mara
kwa mara, hali inayotishia usalama wa afya zao.
"Kwa kweli wanafunzi wana changamoto kubwa na hasa hii ya ukosefu
wa matundu ya kutosha ya choo na kusababisha wajisaidie kwa zamu na tena
sehemu moja bila kujali jinsi yao,” alisema.
Alisema kutokana na uchache wa matundu ya vyoo, wanafunzi wake
walikuwa wakitumia vyoo vya majirani wanaoishi karibu na shule hiyo,
lakini baadaye wakawa wanawafukuza kila wanapokwenda kupata huduma hiyo.
Mwalimu huyo alisema ana uhakika siku chache zijazo tatizo la vyoo
litakwisha kwa kuwa choo cha matundu 10 kinakarabatiwa. Alisema ili
kukidhi mahitaji ya vyoo, shule yake inahitaji matundu 18.
Alisema choo hicho kikikamilika shule yake itakuwa na jumla ya
matundu 14 hivyo kubakia manne ili kukamilisha idadi ya yale
yanaotakiwa.
Alifafanua kuwa mwaka huu shule hiyo imepokea watoto 145 wa darasa
la kwanza 145, hivyo kuifanya kuwa na jumla ya wanafunzi 750, ambao
wanahitaji kupata huduma hiyo muhimu wawapo shuleni.
Ofisa Elimu wa Wilaya ya Tarime, Emmanuel Johnson, alipoulizwa
kuhusu tatizo hilo, alithibitisha na kusema aliamuru shule hiyo ifungwe,
ndipo wananchi wakaanza kushirikiana na uongozi wa shule kukarabati
choo cha zamani.
"Kuna upungufu mkubwa wa vyoo, jamii ya pale haikuwa tayari
kuchangia ujenzi, lakini baada ya kuagiza ifungwe ili kunusuru afya za
wanafunzi, ndipo sasa wananchi wamejitolea kwa hali na mali kukamilisha
choo cha matundu kumi," alisema Johnson.
Alisema kuwa wiki ijayo choo hicho kitakuwa kimekamilika kwa vile
kazi inakwenda kwa kasi kwa ushirikiano kati ya mafundi na baadhi ya
wazazi ili kuhakikisha shule inaondokana na adha hiyo.
CHANZO:
NIPASH.
0 comments:
Post a Comment