Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti mkoani Mara,
Cosmas Qamara (wa pili kushoto), akikamkabidhi seti ya kompyuta Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa wilaya hiyo, Ismael Ngaile, iliyotolewa na kampuni ya
Grumeti Reserves na Grumeti Fund kusaidia shughuli za mahakama hiyo.
Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Naomi Nnko
(kushoto), Mwenyekiti wa Halmashauri, Juma Porini (kulia) na wa tatu
kulia ni Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, Ami Seki.
Mahakama ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara,
imepokea msaada wa vifaa vya kisasa vya Teknolojia, Habari na
Mawasiliamo (Tehama) kutoka kwa kampuni ya utalii ya Singita Grumeti
Reserves Ltd na shirika lake dada la Grumeti Fund.
Vifaa hivyo ikiwamo kompyuta na printa, vilikabidhiwa mwishoni mwa
wiki iliyopita kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Serengeti, Ismael
Ngaile, katika hafla iliyofanyika katika ofisi za mahakama hiyo iliyopo
mjini Mugumu.
Ngaile alishukuru Grumeti kwa kuitikia ombi lao kuwapatia vifaa
hivyo na kuahidi kuvitumia kuboresha huduma katika mahakama hiyo.
“Tulikuwa tunafanya kazi kwa kutumia kompyuta moja, lakini sasa
ufanisi utaongezeka na nakala za hukumu zitatoka mapema kuliko
ilivyokuwa zamani. Hivyo kwa kweli tunashukuru sana,” alisema Ngaile.
Meneja wa Mahusiano wa Singita Grumeti Reserves na Grumeti Fund,
Ami Seki, alisema msaada huo ni sehemu tu ya mchango wanaotoa
kuboresha huduma mbalimbali kwa wananchi wa Wilaya za Serengeti na Bunda
mkoani Mara.
“ Tunaamini kuwa vifaa hivi vitasaidia kurahisisha kazi za kiofisi
na hivyo kuboresha huduma na hii ni sehemu tu ya misaada inayotolewa na
Singita Grumeti Reserves kwa kushirikiana na Grumeti Fund kuboresha
huduma kwa wananchi,” alisema Seki.
Akizungumza katika halfa hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya
Serengeti, Cosmas Qamara, alisema vifaa hivyo vitaiwezesha mahakama hiyo
kufanya kazi kwa kutumia teknolojia ya kisasa na hivyo kuharakisha
upatikanaji wa haki.
“Nina imani sasa wananchi watakuwa wanapata nakala za hukumu ndani
ya wiki moja badala ya miezi mitatu na ni hatua nzuri katika kupata haki
kwa wakati,”, alisema Qamara.
Aidha, aliishukuru Grumeti kwa kuendelea kutoa misaada mbalimbali ambayo inasadia kubadilisha maisha ya wananchi.
“Tunathamini sana juhudi mnazozifanya. Hii siyo mara ya kwanza
kupata msaada kutoka Grumeti. Mmefanya mambo mengi mazuri katika sekta
za elimu, maji na afya,” alisema Qamara.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
ya Wilaya ya Serengeti, Naomi Nnko na Mwenyekiti wa halmashuri hiyo,
Juma Porini.
Viongozi hao pia walisema kampuni ya Grumeti imeonyesha mfano ambao
unapaswa kuigwa na wawekazaji wengine ambao wamewekeza katika wilaya
hiyo.
“Grumeti ni wadau wetu muhimu sana. Wamefanya mambo mengi sana na
wadau wengine wajifunze kutoka kwao”, alisema Mwenyekiti wa Halmashauri
ya Serengeti, Juma Porini.
Uwekezaji katika miradi ya jamii ambao unafanywa na Singita Grumeti
Reserves kwa kushirikiana na Grumeti Fund, unaripotiwa kupunguza
vitendo vya uwindaji katika mapori tengefu ya Ikorongo na Grumeti.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment