Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameeleza kuwa
Serikali itaunda Kamati itakayotathmini kero zinazolalamikiwa na
wananchi wanaozunguka mgodi wa dhahabu wa Acacia North Mara uliopo
wilayani Tarime Mkoa wa Mara, na majina ya Kamati hiyo yatawasilishwa
kwake leo.
Alitoa maamuzi hayo akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani hapa
iliyolenga kutatua kero za wananchi hao, kabla ya kutoa msimamo huo wa
Serikali, alizungumza na makundi mbalimbali ikiwemo wananchi, viongozi
wa wananchi wakiongozwa na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo.
“Baada ya kusikiliza wananchi ambao walieleza kero zao na baadaye
kukutana na mgodi na kuwaeleza malalamiko ya wananchi ambayo mengine
wameyakubali na mengine kuyakataa, sasa ili kutatua suala hili kwanza
lazima tuunde Kamati itakayoangalia kwa undani sehemu zinazolalamikiwa
na kupata vielelezo kabla ya kufanya maamuzi yoyote,” alisema.
Alisema Kamati hiyo itaundwa na wajumbe kutoka Wizara hiyo katika
Idara ya Madini, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Tarime, Mwakilishi wa Mbunge wa
Tarime Vijijini, viongozi wa vijiji na vitongoji vinavyozunguka mgodi
huo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Baraza la Taifa la
Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC).
Kamati hiyo pia itajumuisha Ofisa wa Maji na Mtathmini kutoka
Halmashauri ya Tarime, Wizara ya Ardhi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (Tamisemi), wawakilishi wa mgodi wa Acacia North
Mara.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment