Imeandikwa na Samson Chacha, Tarime
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulongo.
MKUU wa Wilaya Tarime mkoani Mara, Glorius Luoga amepiga marufuku
kusafirisha mifugo usiku wilayani humo, ikiwa ni hatua ya kudhibiti
wimbi la wizi wa mifugo. Aidha, ametangaza vita na wakulima,
wasafirishaji, wauzaji na watumiaji wa bangi kwani matumizi yake,
yamechangia kukithiri uhalifu wilayani humo.
Luoga alisema hayo wakati wa Kongamano lililoandaliwa na kikao cha
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulongo mjini hapa. Kongamano hilo
lilihudhuriwa na viongozi wa serikali, wa kidini na kimila, Polisi
wilaya ya Rorya, wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri na watumishi wa
kawaida.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema kutokana na matukio mengi ya wizi wa
mifugo yanayoibuka kila siku, amepiga marufuku usafirishaji wa mifugo
nyakati za usiku. Alisema usafirishaji huo, unawachanganya wanaoibiwa
mifugo ambayo mingi huibwa usiku.
“Kwa nini mfanyabiashara halali asisafirishe mifugo yake mchana
badala yake asafirishe usiku? Hapo kuna jambo la uhalifu ukiwemo wa
kukwepa kodi na ushuru halali wa Serikali,” alisema Luoga.
Kuhusu bangi, Luoga alisema uongozi wa Wilaya unatangaza vita na
wakulima wa bangi, wasafirishaji na wauzaji wa zao hilo kwani matumizi
yake yamewaathiri vijana wengi wenye nguvu kazi na wamejiingiza katika
uhalifu.
Alisema mwananchi atakayetoa taarifa za siri za kuwepo na mashamba ya
bangi katika eneo fulani na kufanikiwa kukutwa shamba hilo, atapewa
zawadi ya Sh 100,000 papo kwa hapo. Aliwataka wananchi wawafichue watu
hao.
CHANZO: HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment