Imeandikwa na Samson Chacha, Tarime
MAOFISA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wa kituo cha Sirari,
mkoani Mara wamelikamata gari aina ya Scania lenye namba za usajili T
291 CBH, mali ya mfanyabiashara wa jijini Mwanza, Charles Nyamaswa
likiwa na shehena ya bidhaa za magendo.
Baadhi ya bidhaa hizo ni marobota ya vitenge, majora ya vitambaa,
nguo na simu za mkononi, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni
150.
Bidhaa hizo zilikuwa zikiingizwa nchini kupitia mpaka ya Kogaja Shirati bila ya kulipiwa ushuru.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Meneja wa Forodha wa
kituo cha Sirari mpakani, Narcissius Moshi alisema, Aprili 4 maofisa wao
wakiwa doria walipata taarifa ya kuonekana lori hilo likiwa maeneo ya
vijiji vya mpaka wa Kogaja Shirati, wilayani Rorya.
Moshi alisema, aliwaagiza maofisa hao walifuatilie ambapo
walilikamata likiwa linataka kuingia barabara kuu ya lami kuelekea
Mwanza .
“Wahusika wa lori hilo walipoulizwa kuhusiana na bidhaa walizobeba
kama zimelipiwa ushuru, walidai kuwa mzigo walio nao haujalipiwa
ushuru”, alisema na kuongeza kuwa, baada ya hapo aliwaagiza walikamate
lori hilo na kulifikisha kituoni.
Meneja huyo wa TRA Sirari, aliwaasa wafanyabiashara wa mikoa ya Kanda
ya Ziwa Mara, Mwanza , Shinyanga , Kagera , Simiyu, Geita na Tabora
kuachana na biashara ya magendo badala yake wafuate utaratibu wa forodha
na sheria za nchi kwa kulipa kodi bila shuruti.
Alisema kodi inayotozwa ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi hivyo inapaswa kulipwa na kila anayestahili, wakiwemo wafanyabiashara.
“Tunawaonya wanaofanya biashara ya magendo na kuwataka waelewe kuwa
hatutasita kuwakamata na kuwapiga faini pindi tutakapowakamata.
Hatutajali kuwarudisha nyuma kibiashara ikiwa hawatatii sheria
inayowataka walipe kodi”, alisema. Alisema, msako wa bidhaa za magendo
na wakwepa kodi ni endelevu katika maeneo mbalimbali hususan mipakani.
CHANZO: HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment