WANUNUZI wa pamba katika Mkoa wa Mara, wameonywa dhidi ya kuharibu mizani ya kupimia zao hilo kwa lengo la kumpunja mkulima.
Wameambiwa watakaokamatwa wakifanya hivyo, watafungiwa leseni za
kununua zao hilo, pamoja na kushitakiwa kwani wanavunja sheria za nchi.
Hayo ni miongoni mwa maazimio ambayo yaliyotolewa juzi na wadau
mbalimbali wa zao hilo katika kikao cha mkataba wa pamba kilichofanyika
wilayani Bunda, chini ya Mwenyekiti wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara Magesa
Mulongo, aliyewakilishwa na mkuu wa wilaya hiyo, Joshua Mirumbe.
Wadau hao walisema wanunuzi wa zao hilo wamekuwa wakiharibu mizani ya
kupimia zao hilo kwa makusudi, kwa lengo la kumuibia mkulima, hali
ambayo mekuwa ikisababisha wakulima nao kutafuta njia mbadala kwa kuweka
maji na mchanga kwenye pamba yao, ili iweze kuongezeka uzito na hivyo
kaharibu kabisa ubora na usafi wa zao la pamba.
Pia azimio jingine ni kumkamata na kumfikisha mahakamani mkulima
yeyote ambaye anaharibu ubora wa zao hilo kwa kuweka maji au mchanga,
ama vitu vingine ambavyo vinaharibu usafi na ubora wa zao hilo.
“Maazimio yote tuliyopitisha ni kutaka kuhakikisha ubora na usafi wa
zao la pamba unaimarishwa zaidi katika mkoa wetu,” alisema Mirumbe.
Katika kikao hicho, wanunuzi wa zao hilo pia wamesema kuwa kuna changamoto nyingi, ikiwemo ya kuwakopesha wakulima pembejeo.
Ilielezwa kwamba, wakulima wamekuwa wakichangia mfuko wa kuendeleza
pamba kwa kila kilo moja Sh 15, huku wanunuzi nao wakichangia kiasi kama
hicho na kufikia jumla ya Sh 30.
Fedha hizo zimekuwa zikikatwa kwa ajili ya kununua pembejeo na kisha
kuwagawia bure wakulima, badala ya kuwabana wanunuzi kupitia kilimo cha
mkataba.
Chanzo Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment