Na
Lydia Churi- Musoma
Mahakama ya Tanzania
inakusudia kuanzisha Mahakama Kuu katika mkoa wa Mara ambapo ujenzi wa jengo la
mahakama hiyo unatarajiwa kuanza wakati wowote mwaka huu.
Akizungumza leo mjini
Musoma katika ziara yake ya ukaguzi wa shughuli za kimahakama katika kanda ya
Mwanza, Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman alisema mkoa wa
Mara unayo haki ya kuwa na Mahakama Kuu kwa kuwa nia ya Mahakama ni kusogeza
huduma karibu zaidi na wananchi.
Alisema mahakama hiyo
itajengwa kwa haraka na itamalizika katika kipindi cha mwaka moja kwa kuwa
fedha kwa ajili ya ujenzi huo tayari imeshatengwa ambapo nyingine imetokana na
msaada waliopewa kutoka Benki ya Dunia.
Alisema kuanzishwa kwa
mahakama hiyo katika Mkoa wa Mara kutawapa fursa wananchi wa Mara ya kupata
huduma kwa karibu zaidi na pia itasaidia kupunguza kesi zilizoko mahakamani kwa
haraka.
Awali akimkaribisha Jaji
Mkuu ofisini kwake alipomtembelea, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulongo alimwomba
Jaji Mkuu kuanzisha Mahakama Kuu katika mkoa wake kwa kuwa asilimia 55 ya kesi
zote za mauaji katika Mahakama kuu kanda ya Mwanza zinatoka katika mkoa wa Mara
hivyo mkoa huo unayo haki ya kuwa na Mahakama Kuu.
Pamoja na mkoa huo kuwa na
kesi nyingi za mauaji, Mkuu huyo wa mkoa alisema mkoa wa Mara pia unakabiliwa
na kesi nyingi zinazohusu masuala ya ardhi kwa kuwa ni asilimia 38.3 tu ya eneo
zima la mkoa huo ndiyo eneo linalotuwa kwa ajili ya makazi ya watu na shughuli
za maendeleo
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu
na Makazi ya mwaka 2012, Mkoa wa Mara una wakazi zaidi ya milioni 1.3.
Alisema Mkoa wa Mara una
eneo lenye kilometa za mraba 30,150 ambapo asilimia 36 ya eneo hilo ni maji
wakati asilimia 25.7 ni eneo lenye mapori na hifadhi za Taifa ikiwemo mbugaya
wanyama ya Serengeti.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa
aliisifu Mahakama ya Tanzania kwa kufanya kazi yake kwa weledi ya kuzimaliza
kesi zilizohusu mapigano ya koo zilizokuwepo katika siku za nyuma mkoani humo
kwa kuwa zimesaidia maeneo ya mkoa huo kuwa salama hivi sasa na hayaonyeshi
dalili za kujirudia. Aliongeza kuwa eneo la haki likitulia hata masuala ya utawala
yakuwa rahisi.
Jaji mkuu jana amehitimisaha
ziara yake katika kanda ya Mwanza yenye mikoa ya Mara, Geita na Mwanza ambapo
alikuwa akikagua shughuli mbalimbali za kimahakama katika kanda hiyo.
0 comments:
Post a Comment