VIONGOZI wa madhehebu ya dini za Kikristo na Kiislamu zaidi ya 100,
wamekutana katika kongamano na kuwaonya baadhi ya watu wanaotumia mgongo
wa makanisa na misikiti kuhama madhehebu kwa lengo la kuvuruga amani.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi wa kiserikali wakiwa wanane
wa tarafa na wazee mashuhuri wilayani Tarime na Rorya, mkoani Mara, na
wamedhamiria kulinda amani ndani ya nyumba za ibada na nchini kwa
ujumla.
Kwa nyakati tofauti walidai wenye lengo la kuhatarisha amani ni
waumini wanaohamahama madhehebu bila sababu za msingi na kuonya kuhusu
tabia hizo. Walisema miongoni mwa watu hao wamo wanasiasa wanaojipenyeza
katika madhehebu kwa nia ya kutaka kuwagawa wananchi.
Kongamano hilo lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Tarime, liliandaliwa na Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya, Andrew Satta
na kuhudhuriwa na viongozi hao.
Akizungumza katika kongamano hilo, Satta alisema viongozi wa dini
wana umuhimu mkubwa wa kuielimisha jamii katika ibada kwani kumekuwa na
wasio waaminifu walioanza kujitokeza na kujipenyeza katika misikiti na
makanisa kufanya uhalifu.
“Vitendo vya uhalifu kama vilivyojitokeza katika miji ya Mwanza na
Tanga tunavilaani sisi jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya wilaya za Tarime Rorya,” alisema.
Alisema, wanawaomba viongozi wa dini kuwafichua waumini wasio
waaminifu wanaojificha katika madhehebu yao kwa nia ya kufanya uhalifu
ili wakamatwe na kuwahoji.
Alionya watu wasiwaamini wageni bila kuwa na uhakika nao na shughuli
zao na kuwataka watoe taarifa kwa vyombo vya usalama ili hatua
zichukuliwe mapema.
Shehe wa Msikiti Mkuu wa Tarime Mjini, Idd Mohamed alisema, “Kuna
waumini wengi katika misikiti yetu hapa katika wilaya zetu hizi mbili
ambao si raia na wamekuwa wakitoa mahubiri katika misikiti yetu na mengi
ya mahubiri yao yanaonekana kupingwa na waumini wenzao”.
Aliwaomba viongozi wa serikali na wa vyombo vya usalama kufuatilia na
kuchunguza baadhi ya wageni hao ambao hata wao wanashindwa kuwafukuza
kwa kuwa ni kinyume na imani.
Naye Mchungaji John Maguge wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT) Tarime, alisema hivi karibuni kuwa katika lao wakati
wakifungisha ndoa walikuja vijana wawili waliokuwa wamevaa kanzu na
kaptula zilizofika kwenye magoti na kofia na kukaa kimya pembezoni mwa
kanisa.
“Tuliwahoji na kuwaondoa baada ya kugundua kuwa walitaka kuvuruga
kufungwa kwa ndoa hiyo. Tusiwaamini watu tusiowajua wala kuwafahamu
wengine ni hatari kwetu tuchukue tahadhari mapema kabla ya matukio ya
uhalifu,” alisema mchungaji Maguge.
Askofu John wa Kanisa la FPCT, Tarime alisema viongozi wa dini
wanatakiwa kushirikiana na Polisi kwa juhudi zao za kuleta amani kwani
kama hakuna amani hata wao katika madhehebu hawataweza kusali wala
kuleta maendeleo kwa jamii.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment