MWANAFUNZI wa darasa la tatu katika shule ya msingi Azimio, wilayani
Tarime, mkoani Mara, Kareb William (10), amekufa baada ya kuangukiwa na
nyaya za umeme katika mtaa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT),
kata ya Sabasaba, mjini Tarime.
Kamanda wa Polisi wa Tarime/Rorya, Andrew Satta alisema ajali hiyo
ilitokea juzi saa 10 jioni wakati mvua iliponyesha ikiandamana na upepo
ambao uliangusha tawi la mti lililokuwa karibu na nguzo na kusababisha
nyaya za umeme kukatika na kumwangukia mwanafunzi huyo na kusababisha
kifo papo hapo.
“Polisi na wafanyakazi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) walipata
taarifa ya tukio hilo na kujaribu kuwazuia wananchi kutofika karibu na
mwili wa mwanafunzi huyo kabla ya kuondolewa kwenye nyaya hizo za
umeme," alisema.
Wafanyakazi wa Tanesco aliamua kuzima umeme ili kuondoa mwili wa
mwanafunzi huyo aliyekuwa ameshakufa na mwili wake ulipelekwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Tarime kufanyiwa uchunguzi.
Kamanda Satta aliwaasa wazazi kuwaelimisha watoto wao wanapoona nyaya
za umeme zimeanguka chini wasiguse, kwani nyingine huwa zinakuwa na
umeme na kuhatarisha maisha yao, na kuwahimiza walimu kutoa elimu
shuleni kuhusu athari za nyaya za umeme zilizoanguka.
Kaimu Meneja wa Tanesco wilayani Tarime, Jackson Michael,
hakupatikana kuzungumzia suala hilo ambapo wahudumu wa ofisi yake,
walidai amekwenda Nyamongo kwenye mitambo ya umeme njia kuu kutoka Mgodi
wa Acacia North Mara uliopo Nyamongo.
CHANZO GAZETI LAHABARI LEO
0 comments:
Post a Comment