Na. Immaculate Makilika - MAELEZO
BARAZA
la Madiwani ya Halmashauri ya Mji wa Bunda limemfukuza kazi Bw. Eliud
Haonga aliyekuwa mtumishi wa Idara ya Ardhi na Mipango na Mthamini
daraja la pili mapema wiki hii, baada ya kughushi nyaraka ili kujipatia
fedha za malipo ya pango.
Bw. Haonga alipokea fedha za malipo ya pango kiasi cha shilingi milioni saba kutoka kiwanda cha OLAM Tanzania mwezi Juni mwaka huu.
Akizungumza
kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Mkoa wa
Mara, Bi. Janeth Mayanja alisema kuwa Bw. Haonga amekiuka Sheria za
Utumishi wa Umma, kanuni ya 42 na uamuzi uliotolewa na baraza la
madiwani ni sahihi.
Bi.
Janeth alisema “Bw. Eliud Haonga alihifadhi shilingi milioni mbili tu
katika akaunti ya Halmashauri ya Mji wa Bunda na kutumia shilingi
milioni tano kwa matumizi yake binafsi”.
“Maamuzi
haya yamechukuliwa baada ya Kamati ya Uchunguzi kumaliza kazi yake kwa
mujibu wa Sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma.” alisema
Bi. Mayanja.
Aidha,
Bi. Mayanja amewaasa watumishi wa Halmashauri Bunda kujiepusha na
vitendo vinavyoashiria wizi na ubadhirifu, na hatua kali zitachukuliwa
kwa yeyote atakayekiuka maadili ya utumishi wa umma.
0 comments:
Post a Comment