Na. Hassan Mabuye (Kitengo cha Mawasiliano - Wizara ya Ardhi)
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William
Lukuvi akimkabidhi Hati 154 za Kumiliki Ardhi kwa wakazi wa wilaya ya
Bunda Mkoani Mara wakati alipofanya ziara ya siku mbili ya utatuzi wa
Migogoro ya Ardhi mkoani humo.
Lukuvi alitoa hati hizo kwa wananchi wa Wilaya ya Bunda ili
kuwarahisishia wakazi hao utaratibu wa kupata hati zao pale walipo
badala ya kuzifuata Mkoani Mwanza katika ofisi za Kamishana Msaidizi wa
Ardhi Kanda ya Ziwa.
Aidha, Katika ziara hiyo Waziri Lukuvi ametatua migogoro ya
Ardhi ya wananchi wa Musoma mjini na wananchi wa Bunda walio na kero za
migogoro ya ardhi na kuzipatia ufumbuzi pamoja na kupokea vielelezo vya
kero za wananchi zaidi 300 walizoziwasilisha kwa Waziri ili azitolee
maamuzi.
Waziri Lukuvi alikagua nyumba za gharama nafuu zilizojengwa
na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Buhare wilayani Musoma
lenye jumla ya nyumba 50 zinazokaribia kukamilika, ambapo alimtaka
Meneja wa Mradi wa NHC mkoa wa Mara Frank Mambo kukamilisha mradi huo
ndani ya miezi mitatu.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William
Lukuvi anaendelea na Ziara zake za utatuzi wa Migogoro ya Ardhi nchini,
ambayo imejikita zaidi katika kutatua migogoro ya ardhi ya Mikoa ya
kanda ya Magharibi, Kaskazini na ile ya Kanda ya Ziwa hapa nchini.
Aidha, Mhe. Lukuvi baada ya ziara hiyo anatarajiwa kuwasili
mkoani Arusha ambapo pia atatua migogoro ya ardhi inayoukabili mkoa huo
katika wilaya za Arumeru na Karatu.
Hadi sasa Mhe. Lukuvi ndani ya mwezi huu wa Desesmba
ameishatatua migogoro ya ardhi ya Mkoa wa Kigoma na wilaya zake za
Kigoma mjini, Kasulu na Kibondo na katika Mkoa wa Shinyanga na wilaya
zake za Kishapu na Shinyanga mjini na katika mkoa wa Geita amefanya
ziara katika wilayani Chato.
0 comments:
Post a Comment