Na: Genofeva Matemu –
WHUSM
Tarehe: 15/12/2016
Wadau wa sekta ya
filamu na michezo ya kuigiza Mkoani mara wametakiwa kushirikiana kwa pamoja
kuwajibika na kukuza tasnia ya filamu nchini kwa kuzingatia weledi na ubora wakati
wa kuandaa filamu kuanzia uandishi wa miswada ya filamu hadi pale filamu
inapokamilika.
Hayo yamesemwa na
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo wakati wa warsha ya mafunzo
ya kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza leo Mkoani
Mara.
“Tumekua tukitoa
filamu nyingi sana hadi kuifanya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa bara la Afrika katika
kuzalisha wingi wa filamu lakini filamu hizo hazizingatii weledi hivyo kuzifanya
zisiweze kuvuka mipaka ya nchi yetu” amesema Bibi. Fissoo
Akizungumza wakati wa
warsha hiyo Mtendaji Mkuu kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo
(TaSUBa) Dkt. Hubert Makoye amesema kuwa warsha za kuwajengea uwezo wadau wa
filamu ni njia mojawapo ya kuimarisha taaluma na kuinua vipaji hivyo ni vyema
washiriki wakatumia warsha hizo kuvuka hatua na kuwa na vitu vipya vya
kuendeleza tasnia ya filamu nchini.
Naye Rais wa
shirikisho la filamu Tanzania Bw. Simon Mwakifwamba amesema kuwa Serikali imeona
uhitaji wa kuwajengea uwezo wanatasnia wa filamu hivyo ni vyema mafunzo haya
yakachukuliwa kwa mtazamo chanya kwani kumekuwa na changamoto kubwa ya masuala
ya weledi kwa wanatasnia wa filamu nchini inayopelekea kuandaa filamu nyingi
zisizokuwa na ubora hivyo warsha iliyotolewa na Bodi ya filamu Mkoani Mara
imetoa fursa kwa wanatasnia kujengewa uwezo kwenye masuala ya elimu na weledi vitakaowawezesha
kuendana na soko la ushindani la kitaifa
na kimataifa.
Aidha Bw. Mwakifwamba
ameyataka makampuni mbalimbali nchini kujitokeza kuwekeza kwenye masuala ya
filamu nchini kwani filamu ni kiwanda kinachokua kwa kasi na kutoa ajira kwa vijana wengi nchini.
Kwa upande wake
muigizaji kutoka Tanzania Drama and Film Arts Association (TDFAA) Bi. Jaqueline
Frank amesema kuwa wadau wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza wa Mkoa wa Mara
wamekua wakitumia vipaji vyao kuandaa filamu bila ya kuwa na weledi hivyo
mafunzo waliyoyapata yatawasaidia kuboresha kazi zao kwa kuziandaa kwa weledi na
ubora wa hali ya juu na kuziwezesha kuvuka mipaka ya Mkoa wa Mara na hata nchi
za jirani.
0 comments:
Post a Comment