Home » » MAMA MACHEL AISHAURI MARA

MAMA MACHEL AISHAURI MARA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mjane wa Rais wa zamani wa Msumbiji, Graca Machel (katikati) akiwasili mjini Musoma kuanza ziara ya siku tatu mkoani Mara kuangalia maendeleo ya mradi wa kusaidia watoto ambao wako nje ya mfumo wa shule unaotekelezwa na Taasisi ya Graca Machel Trust (GMT) kwa ushirikiano wa Mara Alliance na Mkoa wa Mara. Wanaompokea ni Mwenyekiti wa Mara Alliance, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Michael Msonganzila (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi (kulia). (Picha na Mugini Jacob).
UONGOZI wa mkoa wa Mara umeshauriwa kuona umuhimu wa kuweka mpango shirikishi wa muda mrefu utakaosaidia watoto ambao wapo nje ya mfumo wa shule ndani ya mkoa huo, ili kupata elimu.
Ushauri huo ulitolewa na aliyekuwa mke wa rais wa Msumbiji, Samora Machel, Graca Machel. Graca pia alikuwa mke wa rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Mama Machel alitoa ushauri huo katika mkutano maalumu na wadau ambao ulitumika kutoa matokeo ya utafiti wa watoto ambao wapo nje ya mfumo wa shule.
Utafiti huo umebaini watoto 11,666 wenye umri kati ya miaka saba hadi 17 ambao wako nje ya mfumo ya shule chini ya mradi wa miaka miwili ambao unatekelezwa na taasisi ya Graca Machel Trust (GMT) kwa ushirikiano wa Mara Alliance na serikali ya mkoa wa Mara.
Aidha, baada ya utafiti huo watoto hao wataandikishwa kupata elimu chini ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (Memkwa). Mama Graca alisema lengo la mradi huo ni kusaidia watoto 20,000 ambao wapo ya nje ya mfumo wa shule kwa sababu mbalimbali.
“Tunahitaji mpango wa miaka mitano au 15 ili kuondoa hili tatizo na huu ni mwanzo wa safari kuondoa tatizo la watoto ambao wako nje ya mfumo wa shule”, alisisitiza Mama Graca.
Utafiti huo umefanywa katika halmashauri tano za wilaya za Tarime, Bunda, Butiama na Musoma.
Umeonesha kuwa Wilaya ya Bunda inaongoza kuwa na watoto wengi walio nje ya shule kwa asilimia 33, Tarime (31), Butiama (26) na Musoma (10).
Mkuu wa Kitengo cha utafiti na machapisho wa Taasisi ya Utafiti wa masuala ya Uchumi na Jamii (ESRF) ambao wamefanya utafiti huo Dk Fortunata Makene, alisema utafiti huo ulifanyika nyumba kwa nyumba.
Dk Makene alisema ni muhimu kuwepo na mpango wa kukabiliana na tatizo la ndoa za utotoni katika mkoa huo wa Mara .
Kwa upande wake, mdau wa elimu mkoani humo, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Michael Msonganzila, alisema ni habari njema kuona kuwa GMT, Mara Alliance na Serikali wameungana kusaidia watoto ambao wako nje ya mfumo wa shule chini ya mpango wa Memkwa.
Akizungumza katika hafla hiyo Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Vicent Naano alimhakikishia Graca kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha kuwa tatizo la watoto walio nje ya mfumo wa shule linabaki kuwa historia na kufanya mradi huo kuwa na mafanikio makubwa.
Graca aliwasili mjini Musoma Machi 13 kwa ziara ya siku tatu mkoani Mara kuangalia maendeleo ya mradi wa kusadia watoto ambao wako nje ya mfumo wa shule unaotekelezwa na taasisi yake kwa ushirikiano wa Mara Alliance na Serikali ya Mkoa wa Mara.

CHANZO GAZETI LA HABARI LEO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa