Imeandikwa na Samson Chacha, Tarime
JESHI la Polisi katika Mkoa wa Kipolisi wa Tarime-Rorya,
linawashikilia watu wawili wakazi wa Mtaa wa Nkende mjini Tarime
wakidaiwa kumkata mkono Mkaguzi wa Polisi wa Kituo cha Ngamba Tana-River
cha nchini Kenya, James Mnuve (50), wakati wakimgombania mwanamke.
Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, SACP Henry Mwaibambe, alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo la kukatwa mkono Mkaguzi huyo wa Polisi wa nchini
Kenya. Mwaibambe alidai kuwa tukio hilo lilitokea Julai 13 mchana
katika mtaa wa Nkende mjini Tarime ambapo vijana hao walitenda kosa
hilo. Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Michael Omahe, anayedaiwa
kumtorosha mwanamke huyo, Anne Njeri, kutoka Kenya na kumleta Tanzania
kisha kuishi naye kinyumba huku akisaidiana na rafiki yake, Daniel
Onchiri.
“Mwanamke huyo (Njeri) anadaiwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi pia
na askari James Mnuve na walikuwa wakiishi huko Tana River nchini Kenya,
baada ya kuondoka, Julai 13 mchana askari huyo alimfuatilia kutoka
Kenya hadi Mtaa wa Nkende, Tarime alipokuwa anaishi na kijana
aliyemtorosha (Michael Omahe),” alisema Kamanda.
Akaongeza, “Alipofika Mtaa wa Nkende alimkuta Michael, pamoja na
rafiki yake huyo wakiwa na mwanamke huyo na hapo ndipo ugomvi ulipoanza
kwani askari James alitaka kuondoka na mwanamke huyo na zikazuka vurugu
kubwa na kusababisha Mnuve kukatwa kwa kutumia panga.”
Aidha Kamanada huyo alisema kuwa, “Jeshi la Polisi tulifika kwenye
eneo la tukio mapema na kuweza kuwakamata watuhumiwa wote watatu;
Marandi, Ochiri na mwanamke huyo na kisha tukawahoji kabla ya
kuwafikisha mahakamani huku majeruhi akiwa amepelekwa katika Hospitali
ya Wilaya ya Tarime kwa matibabu.” Gazeti hili lilipomhoji majeruhi
James alidai kuwa yeye ni Inspekta wa Polisi wa Kituo cha Ngamba Tana
River nchini Kenya na mwanamke huyo, Njeri Wanjoi, ni mke wake.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment