WANAFUNZI wawili wa shule ya msingi Sarawe iliyoko tarafa ya Chamriho
halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoani Mara, wamekufa na wengine sita
kujeruhiwa baada ya kuangukiwa ukuta wa chumba cha darasa wakati
wakipembua mahindi kwa ajili ya chakula chao.
Tukio hilo lilitokea juzi majira saa kumi jioni wakati wa saa ya
mapumziko katika eneo la shule hiyo. Wanafunzi waliokufa katika tukio
hilo ni pamoja na Anastazia Wazilana (8) aliyekufa papo hapo na Amosi
Stima Igala (8) aliyekufa wakati akikimbizwa katika hospitali ya rufaa
ya Bugando jijini Mwanza kwa ajili ya matibabu zaidi, ambapo wote
walikuwa wanasoma darasa la pili shuleni hapo.
Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Bunda ,Dk Nuru Yunge
amethibitisha vifo hivyo na kwamba majeruhi walipelekwa kituo cha afya
Ikizu na wengine wamehamishiwa katika hospitali ya DDH Bunda.“Pale kituo
cha afya Ikizu tulipokea majeruhi saba, na wengine wawili
tukawahamishia katika hospitali ya DDH Bunda, kutokana na hali zao kuwa
mbaya, lakini kwa taarifa niliyopata majeruhi mmoja amekufa wakati
akipelekwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando,” alisema.
Ofisa tarafa ya Chamriho Boniphace Maiga, aliwataja wanafunzi
waliojeruhiwa kuwa ni pamoja na Happynes Mussa (13) wa darasa la tano,
Wambura Nyamrosha (12) wa darasa la nne, Sara Wazilana (14) wa darasa la
sita, Emmanuel Mkiriti (8) wa darasa la pili, Mugaya Galinde (8) wa
darasa la pili na Pili Juma Matwiga (7) wa darasa la kwanza.
Maiga alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni ukuta wa darasa hilo kuwa
na ufa wa siku nyingi, ambapo uliporomoka na kuwaangukia wakati
wakianda mahindi kwa ajili ya chakula cha wanafunzi shuleni hapo,
kinachotolewa na shirika la PCI. “Wakati wa mapumziko wanafunzi hao
walikuwa nje ya darasa hilo wakipembua mahindi ya PCI na ghafla ukuta
huo ulidondoka na ulikuwa na ufa mkubwa siku nyingi. Mwanafunzi mmoja
alifia hapo hapo na mwengine amekufa wakati akikimbizwa Bugano baada ya
kuwapatia rufaa,” alisema.
Baadhi ya mashuhuda akiwemo katibu wa huduma za jamii katika serikali
ya kijiji cha Sarawe, Richard Karangi, walilielezea tukio hilo kuwa ni
la kusikitisha, ambapo muuguzi mmoja katika hospitali ya DDH Bunda,
alizungumzia hali ya majeruhi mmoja aliyempokea kwamba inaendelea
vizuri.
Kamanda wa polisi mkoani Mara, Jafari Mohamed hakupatikana
kuzungumzia tukio hilo, lakini polisi wilayani hapa wamethibitisha
kuwepo kwa tukio hilo. Wakati huo huo, baadhi ya wananchi waliozungumza
na waandishi wa habari walisema kuwa ipo haja ya wakaguzi wa shule
kukagua majengo ambayo hayana ubora na kuagiza yasitumiwe na wanafunzi
ili kuepusha majanga kama hayo ambayo siyo ya lazima yasitoke tena.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment