MAPAMBANO ya kutumia silaha za jadi
yakiwemo mapanga kati ya wakazi wa Kijiji cha Wegita na Nkerege
wakituhumiana kuibiana bangi mashambani, yamesababisha vifo vya watu
wawili na wengine wawili kujeruhiwa.
Waliouawa ni Magoro Isaro(35) na Kisyeri Isaro(20) wa kijiji cha Wegita .
Ugomvi kati ya familia ya Mwita Mgaya Kinusu wa kijiji cha Wegita na
familia ya Makanga Kihugi wa Kijiji cha Nkerege baada ya kutuhumiana
kuibiana bangi katika mashamba ya familia ya Makanga, ulithibitishwa na
kamanda wa Polisi Tarime/Rorya.
Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, Henry Mwaibambe amethibitisha kutokea
kwa mauaji hayo na kudai familia ya Makanga ilidai kuibiwa bangi
shambani ekari tatu iliyovunwa usiku na watu wasiojulikana na kuanzisha
vurugu kubwa iliyosababisha vifo.
Aidha ugomvi ulianza, baada ya familia ya Makanga kuhusisha familia ya
Mwita na kuanza kuwashambulia watu waliokuwa wakitoka kijiji cha Wegita
kwa mapanga, mishale na mikuki na kusababisha vifo vya wakazi wa wawili
wa kijiji jirani cha Wegita.
“Katika vurugu hizo mbali na kuuawa watu hao wawili Magoro na Kisyeri,
katika familia ya Makanga watu wake wawili pia nao walijeruhiwa ambao ni
Matinde Makange(44) na Nyakirugi Mirumbe ambao kwa sasa wamelazwa
katika kituo cha afya Wegita wakiwa chini ya ulinzi wa Polisi huku
tukiendelea kuwasaka wote waliohusika katika mauaji hayo,” alisema.
Kamanda Mwaibambe alitoa mwito kwa wakazi wa vijiji hivyo kuacha
kujichukulia sheria mkononi na kwamba inaendesha kufanya msako wa watu
wanaolima mashamba, kuuza na kuvuta banki na kwamba msako huo utakuwa
endelevu katika vijiji vya Wegita, Nyarwana, Nkerege na Kemange
vinavyosifika kwa kilimo hicho haramu.
Mwaka huu tayari zaidi ya ekari 50 zimeteketezwa na kamati ya ulinzi na
usalama katika vijiji hivyo ambapo Kamanda Mwaibambe aliwaonya wakulima
hao kuwa hatua za kisheria na msako wa kuwabaini wakulima hao unaendelea
na kuwataka wananchi kuacha kujihusisha na kilimo hicho haramu na dala
yake walime mazo ya chakula.
IMEANDIKWA NA SAMSON CHACHA- HABARILEO TARIME
0 comments:
Post a Comment