Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (aliyekaa
mbele) akiongea na kutoa maagizo kwa Meneja wa TRA Wilaya ya Bunda
Mkoani Mara pamoja na wafanyakazi wengine wa Mamlaka hiyo kuhusu
ukusanyaji wa mapato ya Serikali mara alipotembelea ofisi ya TRA
Wilayani hapo ili kujionea namna ukusanyaji mapato unavyofanyika mapema 3
Februari, 2018.
Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (kulia)
akimsisitizia jambo Mfanyabiashara wa duka la nguo Wilayani Bunda Mkoani
Mara kuhusu suala la umuhimu wa kutumia mashine ya Kielektroniki ya
Kutolea Risiti (EFD) mara alipofanya ukaguzi wa mashine hizo katika
baadhi ya maduka Wilayani hapo 3 Februari, 2018.
Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (kulia)
akikagua taarifa ya mauzo ya siku ya Mashine ya Kielektroniki ya Kutolea
Risiti (EFD) toka kwa Wafanyabiashara wa duka la vifaa vya nyumbani
Wilayani Bunda Mkoani Mara mara alipofanya ukaguzi wa mashine hizo
katika baadhi ya maduka Wilayani hapo 3 Februari, 2018.
Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere
(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa TRA Wilaya ya
Bunda Mkoani Mara pamoja na wafanyakazi wengine wa Mamlaka hiyo mara
alipotembelea ofisi ya TRA Wilayani hapo ili kujionea namna ukusanyaji
mapato unavyofanyika mapema 3 Februari, 2018.(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-TRA).
Na: Veronica Kazimoto-Bunda,
Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere
amemsimamisha kazi Meneja wa TRA Mkoa wa Mara Ndg. Nicodemus Mwakilembe
kutokana na uzembe wa kutosimamia vizuri matumizi ya Mashine za
Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) kwa wafanyabiashara wa mkoani
kwake.
Uamuzi
huo umetokana na ziara ya kushtukiza ya kukagua matumizi ya EFD
aliyoifanya Kamshina Mkuu wa TRA kwenye baadhi ya maduka ya biashara
Wilayani Bunda Mkoa wa Mara. Akizungumza
mara baada ya ziara yake, Kamishna Mkuu Kichere alisema Meneja huyo
ameonyesha uzembe wa hali ya juu kwani kuna wafanyabishara wengi mkoani
kwake ambao walishalipa fedha kwa ajili ya kupata mashine za EFD lakini
mpaka sasa hawajapatiwa mashine hizo.
"Katika
ziara yangu nimegundua kwamba, wapo wafanyabiashara ambao walikwisha
kulipia mashine tangu mwaka 2013, 2014 na 2015 lakini mpaka sasa bado
hawajapatiwa mashine za EFD na wamekuwa wakitumia mwanya huo kama kinga
ya kutochukuliwa adhabu na TRA wakati Meneja wa Mkoa yupo na hachukui
hatua zozote. Huu ni uzembe uliopitiliza na kamwe siwezi kuuvumilia,"
alisema Kichere.
Kutokana
na uzembe huo, Kamishna Mkuu Kichere amewaagiza Mameneja wote wa TRA
nchi nzima pamoja na majukumu mengine, kuhakikisha wanasimamia
kikamilifu matumizi ya mashine za EFD katika mikoa yao na amesema
hatasita kumuwajibisha Meneja yeyote atakayeshindwa kutekeleza majukumu
yake ipasavyo.
Ziara
hiyo ya kushtukiza imewawezesha wafanyabiashara waliokuwa wamelipia
mashine za EFD miaka ya nyuma, kupata mashine hizo na kufundishwa jinsi
ya kuzitumia ambapo wengine wamejitokeza kununua mashine hizo kwa ajili
ya biashara zao. Kamishna
Mkuu aliongeza kuwa, mashine za EFD zina umuhimu sio tu kwa Serikali
kupata mapato bali kwa wafanyabiashara husika kwani huwawezesha kutunza
kumbukumbu, kujua mwenendo halisi wa biashara zao na hatimaye kulipa
kodi stahiki.
Sambamba
na hayo, Kichere amewataka wananchi wasiishie tu kudai risiti bali
wakishachukua risiti hizo wazikague ili kuthibitisha uhalali wake na
usahihi wa kiasi cha pesa walicholipa. Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania yuko mkoani Mara kwa ziara ya siku 5
ambapo amepata nafasi ya kutembelea Vituo vya Forodha mipakani na ofisi
mbalimbali za mamlaka hiyo pamoja na baadhi ya wafanyabiashara akikagua
matumizi ya mashine za EFD.
0 comments:
Post a Comment