Home » » Kamishna wa TRA amsimamisha kazi Meneja wa Mara

Kamishna wa TRA amsimamisha kazi Meneja wa Mara

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),  Charles Kichere amemsimamisha kazi Meneja wa TRA Mkoa wa Mara  Nicodemus Mwakilembe kwa kushindwa kusimamia vizuri mashine za  Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs).

Uamuzi huo umetokana na ziara ya kushtukiza ya kukagua matumizi ya EFD aliyoifanya Kamshina Mkuu wa Tra kwenye baadhi ya maduka ya biashara Wilayani Bunda Mkoa wa Mara.

Akizungumza mara baada ya ziara yake, Kamishna Mkuu Kichere alisema kuna wafanyabishara wengi mkoani Mara  ambao walishalipa fedha kwa ajili ya kupata mashine za EFD lakini mpaka sasa hawajapatiwa mashine hizo.

"Katika ziara yangu nimegundua kwamba, wapo wafanyabiashara ambao wameshalipia mashine tangu mwaka 2013, 2014 na 2015 lakini mpaka sasa bado hawajapatiwa mashine za EFD na wamekuwa wakitumia mwanya huo kama kinga ya kutochukuliwa adhabu na TRA wakati Meneja wa Mkoa  yupo na hachukui hatua zozote. Huu ni uzembe uliopitiliza na kamwe siwezi kuuvumilia," amesema  Kichere.


Kichere amewaagiza mameneja wote wa TRA nchi nzima pamoja na majukumu mengine, kuhakikisha wanasimamia kikamilifu matumizi ya mashine za EFD katika mikoa yao na amesema hatasita kumuwajibisha meneja yeyote atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Ziara hiyo ya kushtukiza imewawezesha wafanyabiashara waliokuwa wamelipia mashine za EFD miaka ya nyuma, kupata mashine hizo na kufundishwa jinsi ya kuzitumia ambapo wengine wamejitokeza kununua mashine hizo kwa ajili ya biashara zao.

Kamishna  Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania yuko mkoani Mara kwa ziara ya siku tano  ambapo amepata nafasi ya kutembelea Vituo vya Forodha mipakani na ofisi mbalimbali za mamlaka hiyo pamoja na baadhi ya wafanyabiashara akikagua matumizi ya mashine za EFD.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa