Na Ahmed Biseko, Bunda
ASASI ya Nuru ya Maendeleo ya Jinsia (NUMAJI) imeanza mkakati maalumu wa kuhamasisha kilimo cha zao la alizeti wilayani na kuwa zao mbadala la biashara.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Mkurugenzi wa NUMAJI, Macraud Jumbura, katika mdahalo wa ufuatiliaji wa rasilimali za umma.
Alisema asasi yao kwa kushirikiana na wataalamu wa kilimo imefanya utafiti na kubani kuwa alizeti ikilimwa wilayani humo, inastawi vizuri na kutoa mavuno ya kutosha.
“Asasi yetu baada ya kufanya utafiti wa kina kwa kushirikiana na wataalamu wa kilimo, tulibaini kwamba alizeti ikilimwa hapa wilayani Bunda, itastawi na kutoa mavuno mengi, kwa kuwa ardhi na hali ya hewa inaruhusu kabisa, sasa tumeanza kuhamasisha wananchi waweze kulima zao kama zao mbadala la biashara,” alisema Jumbura.
Alisema wakulima badala ya kutegemea kilimo cha zao la pamba kama zao la biashara ambalo bei yake imekuwa haina uhakika zaidi kutokana na kushuka mara kwa mara, sasa hawana budi kuanza kulima alizeti ambalo soko lake ni la uhakika.
Aidha, alisema sasa ni wajibu wa wadau walioshiriki katika mdahalo huo kuhakikisha wanafikisha ujumbe huo kwa wananchi wengine ambao hawakupata fursa hiyo.
Alisema kilimo cha zao la pamba ambalo ni kati ya mazao ya biashara wilayani humo, likiwamo zao la mpunga, kimekuwa hakimnufaishi mkulima kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya ukosefu wa pembejeo na bei yake kutokuwa ya uhakika.
Kwa upande wake, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Bunda, Alistarico Chibhunu, alisema ardhi ya wilaya hiyo pamoja na hali ya hewa inafaa kwa kilimo cha zao la alizeti.
Aliwataka wakulima wilayani humo, kuchangamkia fursa hiyo, badala ya kung’ang’ania kilimo cha zao la pamba ambalo linakabiliwa na changamoto nyingi.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment