na Ahmed Makongo, Bunda
MTOTO mdogo mwenye umri wa miaka mitatu, amenusurika kifo baada ya baba yake kuuawa na wananchi wenye hasira, kisha kuchomwa moto kwa tuhuma za wizi wa ng’ombe wawili, wilayani Bunda, Mara.
Taarifa kutoka Jeshi la Polisi zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea juzi usiku katika kijiji cha Nansimo wilayani hapa, na kwamba mwanaume huyo aliyeuawa ametambulika kwa jina la Shukuran Kajana.
Ilielezwa kuwa siku ya tukio mtu huyo aliyekuwa na wenzie wawili waliiba ng’ombe wawili mali ya mkazi wa kijiji cha Kigaga, wilayani Bunda na kwamba wakiwa katika harakati ya kutaka kusafirisha ng’ombe hao kwa kutumia mtumbwi, ili kwenda kuwauza kwenye kisiwa cha Nafuba ndipo wavuvi walipowakurupusha na kuwapigia yowe.
Taarifa zilieleza kuwa, kutokana na kelele hizo zilizopigwa na wavuvi hao, wananchi wenye hasira kutoka kijiji cha Kigaga na kile cha Nansimo, walifika eneo hilo na kuwafukuza wezi hao, ambapo wawili walikimbia kusikojulikana, na marehemu alikimbilia ndani ya nyumba yake na kujifungia.
Diwani wa kata ya Nansimo Sabato Mafwimbo, alisema kuwa wananchi walimwamuru mtuhumiwa atoke nje, lakini alikaidi amri hiyo na kudai kwamba hata wakija polisi hawezi kutoka ndani ya nyumba hiyo hali iliyowafanya wananchi hao kuichoma moto.
Alisema mtuhumiwa alitoka nje na mtoto baada ya moto huo kuwashwa, ndipo wananchi hao walipompiga hadi kusababisha kufariki.
Imeelezwa kuwa mama wa mtoto huyo alikwishaachana na mwanaume huyo aliyeuawa, kutokana na mtafaruku wa kifamilia uliokuwepo katika ndoa yao.
Tukio hilo limetokea siku moja baada ya wananchi wenye hasira kutoka katika kijiji cha Nakatuba, kumuua mwanaume mmoja, aliyefahamika kwa jina moja la Siku, kwa tuhuma ya kuiba ng’ombe mmoja mali ya mkazi wa kijiji hicho.
Katika tukio hilo wananchi hao pia walichinja ng’ombe 20 na mbuzi 25 kisha kugawana, mali ya Mandela Mboje, mkazi wa kijiji hicho kwa madai kwamba alimtetea mtuhumiwa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment