na Ahmed Makongo, Bunda
MKAZI wa Kijiji cha Mekomariro, wilayani hapa, Nkanga Daudi, amehukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Bunda, kutumikia kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kupatikana na kosa la kumbaka mke wa rafiki yake.
Ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Masoud Mohamed, kuwa Daudi alitenda kosa hilo Julai 26 mwaka 2009, majira ya saa nane mchana nyumbani kwa mlalamikaji.
Masoud alisema kuwa, siku ya tukio mshtakiwa huyo alikwenda nyumbani kwa rafiki yake na kumkuta mwanamke huyo akiwa ndani, na ndipo alipotoa panga alilokuwa nalo na kumlazimisha kufanya naye mapenzi kwa nguvu.
Alisema, kuwa baada ya tendo hilo mtuhumiwa huyo alikimbia lakini mwanamke huyo alipiga yowe la kuomba msaada na ndipo wananchi, ambao baadhi yao walitoa ushahidi mahakamani hapo, walipofika katika eneo la tukio na kushuhudia mtuhumiwa huyo akitimua mbio.
Hakimu Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Joackimu Tiganga, alisema kuwa ameridhika pasipo shaka juu ya ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, hivyo akamuhukumu kifungo cha miaka 30 jela mshitakiwa huyo, na pindi akimaliza adhabu yake, amlipe fidia ya sh 800,000 mlalamikaji.
Wakati huo huo, mwanaume mmoja amehukumiwa na mahakama ya wilaya ya Bunda, kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela, baada ya kukiri kosa la kujihusisha na matukio ya uhalifu wa kuvunja nyumba na kuiba.
Mwendesha Mashtaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Masoud Mohamed, aliieleza mahakama hiyo kuwa Yohana Tilinga (22) mkazi wa kijiji cha Nyatwali, wilayani Bunda, alidaiwa kwamba Agosti 7 mwaka huu, majira ya saa 4 usiku, katika kijiji cha Nyatwali, alikamatwa na wananchi wa kijiji hicho, akiwa na vitu vya kuvunjia nyumba kwa lengo la kufanya uhalifu.
Mohamed alisema kuwa, mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na funguo bandia pamoja na ‘plaizi’ na baada ya kuhojiwa na wananchi, alikiri kwamba vitu hivyo amekuwa akivitumia kuvunjia nyumba yakiwemo maduka na kuiba vitu mbalimbali.
Hakimu Tiganga, alisema kuwa kwa vile mshitakiwa amekiri kosa lake na hakuisumbua mahakama, hivyo anamhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela ili liwe fundisho kwake na kwa wengine wenye nia kama hiyo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment