Home » » HOSPITALI BUNDA YAKITHIRI UCHAFU

HOSPITALI BUNDA YAKITHIRI UCHAFU

na Ahmed Makongo, Bunda
HOSPITALI teule ya Wilaya ya Bunda, inakabiliwa na uchafu uliokithiri kutokana na vyoo vyake kujaa, hali ambayo inasababisha wagonjwa na watu wanaofika hospitalini hapa kujisaidia hovyo na kuharibu mazingira.
Kutokana na hali hiyo Baraza la Mamlaka ya Mji mdogo wa Bunda chini ya Mwenyekiti wake, Pastory Ncheye, jana lilipitisha azimio la kuunda kamati ya kuchunguza hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kupendekeza hospitali hiyo kufungwa, ili kunusuru afya za wananchi.
Wajumbe hao walisema, hospitali hiyo kwa sasa ni chafu ndani na nje hali ambayo huwalazimu wagonjwa na watu mbalimbali wanaofika hospitalini hapo kujisaidia hovyo na kuharibu mazingira, kutokana na vyoo vya hospitali hiyo kujaa na kwamba tayari vimefungwa.
Walisema kuwa, hali hiyo ya kujisaidia hovyo inaweza kusababisha magonjwa ya milipuko, kikiwemo kipindupindu kutokea hospitalini hapo na kusababisha madhara makubwa ya kiafya kwa jamii, na kuiomba idara ya afya kuifunga kabla madhara makubwa hayajatokea.Ofisa Mtendaji wa mji mdogo wa Bunda (TEO), Charles Machage, alisema kuwa mara kwa mara hospitali hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi za kiafya, ikiwemo kukosekan kwa huduma muhimu kama vile mashine ya X-ray.
Alisema kutokana na hali hiyo, wagonjwa wamekuwa wakipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mara mjini Musoma, Hospitali ya Misheni Kibara na Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. William Krekamoo, alikana watu kujisaidia hovyo kama inavyodaiwa, lakini hivi sasa wameanza kuchimba vyoo vingine vya ziada, baada ya vyoo vilivyokuwepo kuziba baada ya kujaa.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa