na Sitta Tumma, Rorya
UONGOZI wa Kanisa Katoliki Parokia ya Ingri, wilayani Rorya, mkoani Mara, umeeleza kufurahishwa kwake na jitihada zilizofanywa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini mkoani humo, Vincent Nyerere (CHADEMA), kuwezesha kupatikana kwa umeme parokiani hapo.
Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Baba Paroko wa Parokia hiyo ya Ingri, Padri Roman Ciupaka, wakati akizungumza kwenye misa ya shukurani iliyofanyika parokiani hapo.
Alisema, miaka michache iliyopita, mbunge huyo wa Musoma Mjini alishirikiana naye kufanikisha kufikishwa kwa huduma ya umeme kanisani hapo, na kwamba ushirikiano huo unapaswa kuigwa na viongozi na watu wengine ndani na nje ya wilaya hiyo.
”Kwa niaba ya kanisa, nakupongeza sana Mheshimiwa Mbunge Nyerere kwa ushirikiano wako mzuri. Umewezesha kupatikana kwa umeme hapa parokiani, nakushukuru wewe pamoja na mke wako, Helen, kwa mioyo yenu mizuri. Asanteni sana na Mungu awabariki milele,” alisema Baba Paroko, Ciupaka.
Kwa mujibu wa Baba Paroko huyo, Ciupaka, Watanzania hawana budi kuiga mfano wa mbunge huyo katika suala zima la kupigania maendeleo yao na taifa kwa ujumla, kwani kufanya hivyo kutachochea madarufu kupiga vita umasikini wa vipato.
Aliwaomba waumini wa kanisa hilo, kujenga tabia nzuri ya kushirikiana na viongozi wao wa dini kwa kuchangia maendeleo ya kanisa, kwani ushirikiano mkubwa ndiyo chachu ya maendeleo, hivyo, ni vema jamii yote ikatambua umuhimu wa maendeleo, badala ya kutegemea misaada kutoka nje ya nchi.
”Jengeeni tabia ya kuchangia maendeleo yenu. Msitegemee misaada kutoka mataifa ya nje ya nchi....kanisa hili ni lenu, nchi hii ni yenu na maendeleo yatakayopatikana ni yenu nyote.
Mimi nataka kwenda Ulaya kwetu Poland, lakini nawaomba sana mpende kuchangia maendeleo,” alisema Baba Paroko huyo ambaye ni raia wa nchi ya Poland.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Musoma, Kisurura, aliwaomba waumini wa kanisa hilo na raia wote wa Wilaya ya Rorya kuanzisha miradi mbali mbali ya uzalishaji mali, ukiwemo ufugaji wa kuku na kilimo cha kisasa, kwani miradi hiyo itaweza kuwapatia maendeleo makubwa na kukuza uchumi wao.
Alisema, kilimo cha kisasa pamoja na ufugaji wa kuku ni njia mojawapo ya kuwakomboa na lindi kubwa la umaskini wa vipato, hivyo ni vema wakachangamkia fursa hizo kwa faida yao na taifa la Tanzania kwa ujumla.
”Ndugu zanguni wananchi wa Rorya, ufugaji wa kuku pamoja na kilimo cha kisasa ndivyo vitu vinavyolipa kwa sasa. Anzeni kufuga na kulima mazao ya biashara na chakula.
”Leo hii mngekuwa na miradi yenu ya kujipatia fedha, msingekuwa mnalalamika na kukosa fedha za kuchangia kanisa. Maendeleo yatakuja pale tu mtu au watu wanapojituma na kubuni mambo ya kuwaingizia fedha nyingi,” alisema meya huyo wa Manispaa ya Musoma, Kisurura.
Naye mbunge wa Musoma Mjini mkoani Mara, Nyerere alitumia muda huo kuwahimiza wananchi wa Rorya na taifa kwa ujumla kushiriki kikamilifu kuhesabiwa katika zoezi la Sensa inayotarajiwa kufanyika Kitaifa Agosti 26, na kwamba mambo hayo mawili ni muhimu sana kwenye maendeleo yao na taifa zima kwa ujumla.
Alisema, wananchi wa Rorya na viunga vyake vyote wahakikishe wanahesabiwa ili serikali iweze kuwa na takwimu zitakazowezesha kuweka mipango thabiti ya kimaendeleo kwa wananchi wake.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment