Home »
» MARA KUSAKA WAVUVI HARAMU ZIWA VICTORIA
MARA KUSAKA WAVUVI HARAMU ZIWA VICTORIA
Na Shomari Binda, Musoma
Kufuatia kuongezeka kwa uvuvi haramu katika ziwa victoria kitengo cha udhibiti uvuvi haramu kanda ya Mara kimeanzisha doria maalumu ya kupambana na watu wanaojihusisha na uvuvi haramu na uuzaji wa nyavu na makokoro ya kuvulia samaki katika ziwa Victoria.
Akiongea na waandishi wa habari baada ya kuwakamata watu wanaojihusisha na uvuvi haramu wakiwa na samaki wadogo tani 3 na nyavu haramu zinazotumika kuvulia samaki wadogo Afisa Mfawidhi Mdhibiti na Doria Kanda ya Mara Braison Meela alisema kikosi cha udhibititi kitaendelea na msako huo kwa muda wote.
Alisema msako huo utaendelea katika maeneo mbalimbali ikiwemo maduka ya wafanyabiashara wanaouza nyavu ili kuona mianya inayoingiza nyavu haramu katika mkoa wa Mara.
Braison alisema licha ya Serikali kupiga marufu vitendo hivyo bado kuna watu wasio waaminifu ambao wanaendeleza shughuli za uvuvi haramu kwa kutumia nyavu zisizoruhusiwa.
Alisema ili kufanikisha zoezi hilo aliwaomba wananchi wema kuendelea kutoa taarifa katika kikosi hicho ili kusaidia kupatika kwa watu wanaojihusisha na uvuvi haramu ili waweze kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria kwani wamekuwa wakisababisha upotevu wa raslimali za Taifa.
Kwa upande wake Afisa Oparesheni Doria na Uvuvi Kanda ya Ziwa Ally Mzee Said alisema oparesheni hizo zitakuwa endelevu kwani kikosi kimejipanga kuihakikisha kina komesha uvuvi haramu mkoani Mara.
Alisema wale wote wanaojishughulisha na masuala ya uvivi haramu waache mara moja na kusalimisha bidhaa wanazozitumia ili kujiepusha na matatizo ambayo watayapata kutokana na Serikali kujipanga vizuri kuhakikisha inakomesha shughuli hizo na kuwafikisha Mahakamani wale wote watakaopatikana na hatia.
Kikosi cha doria na udhibiti wa uvuvi haramu mkoani Mara ni moja ya vikosi vilivyopo katika mikoa minne iliyopo katika ziwa Victoria vinavyopambana na shughuli za uvuvi haramu.
Kikosi hicho awali kimekuwa kikikabiliwa na ukata wa vitendea kazi kwa ajili ya kupambana na uvuvi haramu ikiwa ni pamoja na magari mafuta na fedha kwa ajili ya shughuli hiyo hali inayosababisha zoezi hilo kuwa gumu.
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment