na Ali Lityawi, Tarime
MBUNGE wa Jimbo la Kisarawe mkoani Pwani, Selemani Jafo amejikuta akibubujikwa na machozi katika mgodi wa dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na Kampuni ya African Barrick Gold Mines baada ya kuelezwa mazingira magumu yanayowakabili watumishi na kuhatarisha maisha yao ya baadaye.
Jafo ambaye anazungukia migodini kwa lengo la kupata maoni ya wafanyakazi wanaopinga sheria ya kuwazuia kuchukua fedha katika mifuko ya pensheni hadi watakapofikisha umri wa kustaafu, alijikuta akikumbwa na adha hiyo juzi wakati akiwa ametembelea mgodini hapo.
Wakizugumza na mbunge huyo, watumishi wa mgodi huo walidai kuwa shughuli wanazozifanya ni ngumu huku mishahara yake ikiwa hailingani na dhoruba zake ambazo wengi wao zimewasababishia ndoa zao kuvunjika kutokana na kuathiri uwezo wa unyumba huku hivi sasa wakikabiliwa na tishio la fao la kujitoa.
Wafanyakazi hao wanaohusika na shughuli za uzalishaji kwa kulipua miamba kwa kutumia kemikali ambazo ni sumu walimuelezea mbunge huyo kuwa sheria hiyo kwao ni kandamizi hasa kwa kuwa ajira yao katika sekta binafsi haina ulinzi tofauti na sekta ya umma.
“Wenzetu wa sekta ya umma, si rahisi kufukuzwa kazi hadi vipite vikao vitakavyotanguliwa na tume ya uchunguzi, lakini sisi ulinzi huo hatuna kwani hata afya yako ikitetereka tu mwajiri anakutimua kazi na tegemeo kubakia katika mafao yako ambayo leo yanawekewa masharti yenye dhamira ya kutuondoa duniani mapema mara baada ya ukomo wa vibarua vyetu,” alisema Mwerema Chambiri “Operator” wa mtambo wa kuchimba vifusi vya madini.
Aidha, wafanyakazi hao waliishutumu serikali kuipitisha sheria hiyo pasipo kuwashirikisha walengwa ambao imeshindwa kuwashawishi kuitumikia kutokana na kutokuwa na uwiano mzuri wa thamani ya fedha pindi wanapofikia ukomo wa ajira na kipindi watakacholazimika kulipwa.
“Nashangaa serikali kutuletea sheria hii kandamizi, haituonei huruma hata sisi wanawake ambao tunawajibika kusimama masaa kumi na mbili katika utumishi wenye mazingira mgumu, tunajiwekea malengo ya kudumu katika kazi hizi kwa muda fulani kwa usalama wa afya zetu, lakini inatuingiza katika kifungo hiki cha ajabu,” alisema na kuongeza:
“Fedha zetu zinabakia na thamani ileile huku kila baada ya muda fulani thamani ya shilingi yetu inashuka na mazingira ya mgodini ni yaleyale hivyo sheria hiyo ni vyema ifutwe,” alisema Asimwe Kafrika, mtafiti wa miamba ya madini huku akibubujikwa na machozi.
Akiongelea suala hilo, Mbunge Jafo alisema dhamira yake ya kuwasilisha hoja binafsi kupinga sheria hiyo iko palepale hasa baada ya kubaini imewagusa Watanzania wengi katika sekta binafsi na sekta ya umma huku akiwatia moyo kwamba imefikia hatua nzuri hasa kwa kuwa hivi sasa inasubiri maamuzi ya Kamati ya Uongozi ya Bunge kuipangia siku ya kuiwasilisha.
Alisema amelazimika kutembelea katika migodi kukusanya maoni zaidi ili kuipatia uzito hoja yake hiyo siku ya kuiwasilisha na katika ziara yake hiyo amejifunza ugumu unaowakabili watumishi wa sekta binafsi ambao mazingira ya kazi yao ni hatarishi hususan wanaofanya kazi za uzalishaji chini ya ardhi.
“Suala la fao la kujitoa si vyema kuliweka katika mzani mmoja baina ya sekta binafsi na umma kutokana na mazingira kuwa tofauti ya uwajibikaji wao,” alisema Jafo.
Aidha alibaini watumishi wa serikali kutofuata taratibu stahiki za kuwashirikisha wadau katika kupata maoni na kuwaelimisha kwa masuala mbalimbali likiwemo hilo la sheria ya fao la kujitoa hivyo kusababisha kuibuka migogoro inayoyumbisha na kuathiri pato na uchumi wa taifa hata kama lina manufaa kutokana na walengwa kutokuwa na ufahamu nalo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment